“We are like many pellets of incense falling on the same altar. Some collapse sooner, others later, but it makes no difference.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.15
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNA MENGI YA KUFANYA…
Kabla hujapoteza muda wako kujilinganisha na watu wengine, kumbuka kwamba una mengi ya kufanya.
Hivyo peleka muda na nguvu zako kwenye hayo muhimu zaidi kwako kufanya.
Kujilinganisha na wengine ni kupoteza muda wako kwa sababu mwisho wa siku hakuna tofauti kubwa baina yetu.
Hakuna tofauti kubwa kati ya mtu mfupi na mrefu, tajiri na masikini, maarufu na asiye maarufu.
Kwa sababu mwisho wa siku hatima yetu ni moja, kifo kitatuweka sawa wote.
Mwisho wa siku wote tutakufa na tofauti zozote za nje tunazohangaika nazo sasa hazitakuwa na maana baada ya kufa.
Bali kitakachokuwa na maana ni kile ambacho umefanya, namna ambavyo umegusa maisha ya wengine.
Ndiyo maana unapaswa kuelekeza nguvu zako eneo sahihi, siyo kwenye kujilinganisha na wengine, bali kwenye kufanya kilicho sahihi na bora, ambacho kitaacha alama kwa watu wengine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokupoteza muda kwenye kujilinganisha, badala yake kuweka muda kwenye yale yaliyo muhimu, kama kufanya kile kinachoongeza thamani kwenye maisha ya wengine.
#UsisumbukeNaKujilinganisha #KifoKitatuwekaSawa #GusaMaishaYaWengine
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1