Rafiki yangu mpendwa,
Maisha ni shule na changamoto tunazokutana nazo ndiyo mtihani wa kutoka darasa moja kwenda jingine. Ukiweza kutatua changamoto moja uliyonayo changamoto kubwa zaidi inakusubiria. Ukishindwa kutatua changamoto uliyonayo utabaki pale ulipo sasa mpaka utakapoitatua. Changamoto hazitakoma kwenye maisha, na ndiyo maana kwenye AMKA MTANZANIA tumeweka kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa.
Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kushauriana kwa kina jinsi unavyoweza kuanzisha biashara yenye mafanikio makubwa ukiwa umeajiriwa, hata kama huna mtaji wa kuanzia.
Kipato cha mshahara kimekuwa kidogo na ambacho hakikui kwa kasi kulingana na ukuaji wa gharama za maisha. Hivyo wengi wamekuwa wakiangalia njia mbadala za kuongeza kipato hicho. Lakini kwa kukosa maarifa na miongozo sahihi, wengi wamekuwa wanashindwa kwenye mambo mbalimbali wanayojaribu.
Wapo wasomaji wenzetu ambao wameomba ushauri kuhusu kuanzisha biashara wakiwa kwenye ajira, na hapa tunakwenda kujifunza kwa kina kuhusu changamoto zao na hatua ambazo wote wanaopitia changamoto kama hizo wanaweza kuchukua.
Nafanya kazi nalipwa laki mbili kwa mwezi na hapa nina miaka minne, lakini naona kwa mshahara huu sitaweza kufikia malengo yangu, nifanye nini ili niweze kuachana na kazi hii? Nafikiria kuanza biashara lakini sijawahi hata kuuza pipi nifanye nini na mtaji wangu ni milioni moja tu. – Victor E. Y.
Ni mtumishi hivyo naweza kupata mkopo hata wa milioni 4 kwa mwaka kesho. Na ninaishi mkoa wa Kagera wilayani, natamani kufanya biashara anayoweza kusimamia mke wangu yenye angalau faida ya 20,000/30,000 kila siku. Nifanye ipi wadau? Naomba msaada wenu ili nijikwamue. – Shedrack E. R.
Nataka niache ajira nianze biashara ya mitumba sijui nianzie wapi. – Brenda E. O.
Kama ambavyo wasomaji wenzetu wameeleza hapo juu, wote changamoto kuu ni moja, kutengeneza kipato zaidi wakiwa kwenye ajira.
Katika kutatua changamoto hiyo kuu, kuna vikwazo mbalimbali wanakutana navyo, ambavyo ni kukosa wazo bora, kukoa uzoefu na kukosa mtaji.
Zifuatazo ni hatua ambazo kila aliyekwama kwenye changamoto ya aina hii anaweza kuzichukua, akaweza kuwa na biashara yenye mafanikio makubwa huku akiendelea na ajira yake.
- USIACHE AJIRA.
Kwanza kabisa, kama upo kwenye ajira na unataka kuanza biashara, basi usiache ajira yako. Badala yake anzisha biashara yako huku ukiendelea na ajira yako. Kwa kufanya hivyo utakuwa na manufaa makubwa ya kuweza kuanzisha na kukuza biashara yako bila ya kuitegemea moja kwa moja kwa sababu una kipato cha mshahara cha kukuwezesha kuendesha maisha yako.
Ila hapa utahitaji kujitoa zaidi, utapaswa kuwa na siku mbili ndani ya siku moja. Utakuwa na siku unayompa mwajiri wako (masaa ya kazi) na siku ya kuipa biashara yako (muda wa kuwa kwenye biashara). Na ninashauri kama unampa mwajiri wako masaa 8 kila siku, basi ipe biashara yako angalau masaa 6 kila siku, kitu ambacho kinawezekana sana kama utajipanga vizuri na ukajifunza kama nitakavyoendelea kukushauri.
- ANZA NA TATIZO.
Kikwazo kwa wengi wanapofikiria kuingia kwenye biashara wakiwa kwenye ajira kimekuwa ni biashara gani wafanye. Wengi huwa wanakwama kwenye wazo lipi ni sahihi kwao, wanaweza kuwa na mawazo mengi na yote wanaona ni mazuri, ila hawawezi kufanya maamuzi waanze na wazo lipi.
Hapa ushauri ni huu, anza na tatizo ambalo watu wanalo. Inaweza kuwa ni watu unaoishi nao eneo moja, watu unaofanya nao kazi au hata mwajiri wako. Kazi yako wewe ni kuangalia ni tatizo gani ambalo wewe mwenyewe unalo au wale wanaokuzunguka wanalo na unaweza kulitatua na kugeuza hilo kuwa wazo lako la biashara.
Watu wana matatizo, na hayo matatizo yao ndiyo mawazo ya biashara, anza kuyaangalia mawazo ya watu na utaziona biashara nyingi unazoweza kufanya. Chagua moja na anza nayo.
- ANZA KIDOGO.
Ukishapata wazo kwa kuanza na tatizo ambalo watu tayari wanalo, wengi wanakwama kwenye kuanza. Ndiyo wazo wanaweza kuwa nalo, lakini inapofika kwenye kuanza, wengi hushindwa.
Na sababu hapa huwa hazikosekani, kutokuwa tayari na kubwa zaidi, kutokuwa na mtaji.
Jawabu ni kuanza kidogo, kuanza kwa hatua za chini kabisa, popote pale unapoweza kuanzia sasa.
Hakuna kitu kizuri kama kuanzia biashara chini, kwa sababu unakuwa ni wakati mzuri sana kwako kujifunza kuhusu biashara hiyo na kuielewa kwa undani. Lakini pia unaepuka hatari ya kupata hasara kubwa kama ukianza na mtaji mkubwa.
Kama wazo ulilopata unaweza kutumia ujuzi wako, uzoefu wako au mtandao wako kutoa huduma kwa wateja wako, basi fanya hivyo.
Kama unahitaji mtaji wa fedha kuanza, anza na mtaji kidogo kabisa ambao unaweza kuanza nao. Jua kiwango hicho cha mtaji na anza kujiwekea akiba kwa ajili ya kuweza kuanza.
Kwa mwanzoni, epuka sana kuchukua mkopo kwa ajili ya kuanza biashara, kuna changamoto nyingi ambazo zinaweza kukuyumbisha sana na ukapoteza vyote, mkopo na biashara pia.
- JIFUNZE KILA SIKU NA PIGA HATUA.
Unapoanza biashara yako kwa hatua ndogo, lengo lako ni kukua zaidi ya pale ulipoanzia. Lakini wengi wamekuwa hawakui, biashara zinabaki pale zilipoanzia, zinadumaa na nyingine kufa kabisa. Kinachopelekea biashara nyingi kuwa kwenye hali hiyo ni wafanyabiashara kutokujifunza.
Biashara ni darasa la maisha, ni eneo ambalo unapaswa kujifunza na kupiga hatua kila siku. Na unapoanzia chini, kitu pekee cha kukuwezesha kupiga hatua zaidi ni kasi yako ya kujifunza.
Jifunze na kila unachojifunza kiweke kwenye matendo. Mfano jifunze mbinu za kuongeza wateja kwenye biashara yako, kisa zifanyie kazi ili uweze kuongeza wateja. Jifunze kuongeza mauzo na weka kwenye matendo uone mauzo yako yakikua zaidi.
Kadiri unayojifunza, ndivyo unavyokuwa bora na biashara yako kukua zaidi.
- IPE BIASHARA NAFASI YA KUKUA.
Biashara nyingi ndogo zimekuwa zinadumaa na kufa kutokana na waanzilishi wa biashara hizo kuanza kuzitegemea biashara hizo mapema. Ndiyo maana nimeanza kwa kushauri usiache kazi yako. Kazi itakusaidia upate fedha zakuendesha biashara yako huku ukiipa biashara yako nafasi ya kukua kwa kutokuondoa fedha kwenye biashara.
Faida unayoipata kwenye biashara unapaswa kuiwekeza kwenye biashara hiyo ili iweze kukua zaidi.
- SOMA KITABU CHA BIASHARA NDANI YA AJIRA.
Niliyokushirikisha hapa ni machache sana kati ya mengi unayopaswa kuyajua ili uweze kuanzisha biashara na kufanikiwa ukiwa kwenye ajira yako.
Nimetoa kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA Toleo la pili, ambalo lina shuhuda za wengi ambao wameweza kuanza biashara wakiwa kwenye ajira na kupiga hatua.
Pia kwenye kitabu kuna michanganuo ya biashara 12 ambazo unaweza kuanza, kwa mifano kabisa kutoka kwa wale wanaofanya biashara hizo. Zipo biashara ambazo hazihitaji kuanza na mtaji, za mtaji kidogo, mtaji wa kati na mtaji mkubwa.
Pata nakala ya kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA leo na huo utakuwa mwongozo wako katika kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa umeajiriwa.
Kupata kitabu cha biashara ndani ya ajira, piga simu au tuma ujumbe kwenda namba 0678 977 007 au 0752 977 170 na utapewa maelekezo ya kukipata.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
Aksante sana Kocha! Unatusaidia sana
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike
ASANTE SANA KOMAKYA SEC MEMBER IMENISAIDIA SANA
LikeLike