“Kwa kufanya kazi kwa uaminifu masaa 8 kwa siku, unaweza kupandishwa cheo na kuwa bosi na kufanya kazi masaa 12 kwa siku” – Robert Frost

“Kwa kufanikiwa kuondoka kwenye ajira uliyokuwa unafanya kazi masaa 8 kwa siku, unaweza kuanzisha biashara ambayo itakutaka kufanya kazi masaa 12 kwa siku.” – Kocha Dr Makirita Amani.

Rafiki yangu mpendwa,

Walioajiriwa na wale waliojiajiri hawana tofauti kubwa sana, kwa sababu wengi wao wanakosa vitu vitatu muhimu sana ambavyo kila mtu anapigania kwenye maisha yake.

Iko hivi rafiki, mtu anapokuwa kwenye ajira, anakosa uhuru wa fedha, kwa sababu kipato kinapangwa na mwingine, anakosa uhuru wa muda, kwa sababu anapaswa kuwa kazini kila siku. Na pia anakosa uhuru wa maisha, hawezi kuchagua kufanya yale anayopenda kwenye maisha yake au kwenda anakotaka, ajira inamtaka kukaa eneo moja.

Mtu huyo huyo akichoka kazi na kuona inamnyima uhuru na hivyo kwenda kujiajiri, anajikuta bado anakosa uhuru wa kipato, kwa sababu anakuwa hajatengeneza wateja wa kutosha, anakosa uhuru wa muda kwa sababu biashara yake inamtegemea yeye kwa kila kitu. Pia anakosa uhuru wa maisha kwa sababu hawezi kuondoka na kuiacha biashara yake.

Tim Ferris anasema hii siyo njia sahihi ya kuyaishi maisha yetu, hatupaswi kuishi kama watumwa tukiamini mambo yatakuwa mazuri baadaye. Anaamini kama mtu huwezi kuchagua kuwa huru sasa, basi hutakuja kuwa huru kwenye maisha yako. Kwa sababu utakachofanya ni kutoka chini ya utumwa wa aina moja kwenda kwenye utumwa wa aina nyingine.

The-4-Hour-Work-Week.jpg

Kwenye kitabu chake kinachoitwa 4-HOUR WORKWEEK, Tim Ferris ameshirikisha hatua nne za kutengeneza uhuru kamili wa maisha yako kwenye fedha, muda na hata eneo.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza sheria kumi ambazo ukizijua na kuziishi utaweza kuwa na uhuru kamili wa maisha yako. Sheria hizi tumeshirikishwa na Tim Ferris kwenye kitabu chake cha 4-HOUR WORKWEEK.

Karibu sana tujifunze sheria hizi kumi, tuziweke kwenye maisha yetu na tuweze kupiga hatua.

MOJA; KUSTAAFU NI MPANGO WA MWISHO.

Ahadi ya ajira ni kwamba utafanya kazi na kisha utakapofika miaka 60 basi utastaafu na kupata mafao yako. Ahadi hii ambayo imekuwa siyo sahihi imewahadaa wengi na kuahirisha kuishi maisha yao sasa kwa kusubiri mpaka watakapostaafu. Na pale wanapostaafu ndiyo wanapokutana na uhalisia kwamba kustaafu huko hakuwapi uhuru ambao walikuwa wanautegemea.

Tim Ferris anatuambia tunapaswa kuweka kustaafu kama mpango wa mwisho kabisa, yaani pale kila kitu kinaposhindwa au tunapojikuta kwenye wakati mgumu, basi mpango wa kustaafu ndiyo utusaidia.

Lakini katika nyakati nyingine, anatuambia tunapaswa kuyapangilia maisha yetu na kuweza kupata mapumziko tunayotaka sasa na siyo kusubiri mpaka mtu utakapostaafu.

MBILI; RIBA NA NGUVU VINAENDA KWA MZUNGUKO.

Huwa tunafikiri kwamba tuna nguvu ya kufanya kazi mfululizo mpaka pale tutakapostaafu na kisha kupata nafasi ya kupumzika. Lakini hivyo sivyo miili yetu binadamu inavyofanya kazi. Kanuni ya asili ni mzunguko, kwenye kila kitu kuna kupanda nakushuka, kuwa juu na kuwa chini. Kadhalika kwa mwili, kuna wakati unakuwa na nguvu ya kufanya kazi na wakati unakuwa hauna nguvu na kushindwa kufanya kazi.

Yatengeneze maisha yako kwa namba kwamba unatumia muda ambao una nguvu kufanya kazi muhimu, na muda ambao huna nguvu kupumzika. Ukipunguza yale ambayo hayana umuhimu kwako, utaweza kwenda vizuri na mwili wako.

TATU; KUFANYA MACHACHE SIYO UVIVU.

Jamii yetu inapima uhodari kwa mambo mengi ambayo mtu anafanya. Huku anayefanya machache muhimu akionekana ni mvivu, anayefanya mengi na yasiyo muhimu anaonekana ni mpambanaji.

Unachopaswa kufanya ni kuchagua majukumu machache muhimu na yenye tija na kufanya hayo, huku yasiyo muhimu ukiachana nacho. Huu siyo uvivu, bali ni matumizi bora ya muda na nguvu zako, ambavyo vyote vina ukomo.

Muda unaopoteza sasa kwenye mambo yasiyo muhimu unayofanya kwenye kazi au biashara yako ni muda unaoweza kuuokoa na kupata uhuru mkubwa wa maisha yako.

NNE; HAKUNA MUDA SAHIHI.

Kama kuna kitu unataka kuanza na kuahirisha kwa kujiambia muda haujawa sahihi jua hili, hakuna muda sahihi zaidi ya muda ulionao sasa. Hakuna wakati ambapo utajiambia uko tayari kuanza, kila wakati utaona kuna kitu kinakosekana.

Kama unajiambia huwezi kutoka nyumbani kwako na kwenda kwenye shughuli zako mpaka taa zote za barabarani ziwake kijani unajichelewesha. Unachopaswa kufanya ni kuanza, kuanza na kile kilicho mbele yako na kisha kuendelea kulingana na yale unayokabiliana nayo.

Chochote unachotaka kuanza, muda sahihi wa kufanya hivyo ni sasa, kesho haitakuwa tofauti sana na ilivyo leo, hivyo usiendelee kujichelewesha.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Yenye Mafanikio Makubwa Ukiwa Umeajiriwa, Hata Kama Huna Mtaji.

TANO; OMBA MSAMAHA NA SIYO RUHUSA.

Iko hivi rafiki, kama kuna jambo ambalo unataka kufanya na inabidi upate ruhusa kutoka kwa mtu mwingine, ukiomba ruhusa hutapewa. Hii ni kwa sababu wengi huwa hawapendi ufanye vitu ambavyo ni vigumu kwako, na hilo linakufanya wewe ushindwe kupiga hatua.

Unachopaswa kufanya ni kufanya bila ya kuomba ruhusa, na pale unapogundulika unaomba msamaha. Hakuna mtu ambaye atakataa msamaha wako, na pale unapokuwa umeshaanza kufanya, hakuna atakayeweza kukuzuia.

Watu watakuzuia kabla hujaanza, lakini ukishaanza wanakosa nguvu ya kukuzuia, hivyo kama kuna jambo muhimu unataka kufanya, usiombe ruhusa, anza kufanya na baadaye una nafasi ya kuomba msamaha kama mambo hayatakwenda vizuri. Lakini pia unakuwa na nafasi ya kupata matokeo bora.

SITA; KAZANA NA UIMARA WAKO NA SIYO MAPUNGUFU YAKO.

Kila mtu ana uimara kwenye maeneo machache ya maisha yake, halafu ana udhaifu kwenye mambo mengi sana. Jamii imekuwa inatudanganya kwamba tunapaswa kufanyia kazi mapungufu yetu ili yasiwe kikwazo kwetu. Na hapo ndipo tunapoharibu zaidi, kwa sababu kila unapojaribu kufanyia kazi mapungufu yako, unayapa nguvu zaidi.

Unachopaswa kujua ni uimara wako uko kwenye maeneo gani kisha peleka nguvu zako kwenye uimara wako. Pia jua mapungufu yako na achana nayo, usihangaike kuyabadili, hutaweza na utayafanya kuwa na nguvu zaidi.

Tumia nguvu zako kwenye yale maeneo ambayo uko vizuri na siyo kwenye maeneo ambayo una udhaifu. Jua uimara wako uko wapi na ufanyie kazi, hapo ndipo utaweza kufanya machache yenye tija na kupata uhuru mkubwa wa maisha yako.

SABA; ZIADA INAKUWA KINYUME.

Vitu huwa vinakuwa vizuri pale vinapokuwa kwa kiasi, lakini chochote ambacho kinazidi kiwango huwa kinageuka na kuwa kibaya. Hivyo ziada ya kitu chochote kile inaleta matokeo ambayo ni kinyume na tunayotaka au kutarajia.

Wapinga ukandamizaji hugeuka kuwa wakandamizaji. Wapigania uhuru huishia kuwa madikteta. Baraka zinapokuja kwa wingi zinageuka kuwa laana. Msaada unapouwa mwingi unakuwa kikwazo. Chochote kinachoatikana kwa wingi kinakosa thamani.

Hivyo kwenye maisha yako, usikazane tu kuwa na vitu vingi, maana mwisho wa siku vinakosa maana ambayo ulitaka. Hata unapokuwa na muda mwingi, unageuka kuwa uharibifu kwako.

Uhuru tunaoutafuta kwenye maisha yetu siyo kwa ajili ya kuutumia vibaya, bali kwa ajili ya kuwa na kiasi na kuutumia vizuri. Kuwa makini sana na hili la wingi, wengi huwa hawaelewi madhara yake mpaka pale yanapowafika.

NANE; FEDHA PEKEE SIYO SULUHISHO.

Watu wengi ambao hawana uhuru kwenye maisha yao huwa wanadhani kwamba tatizo ni fedha, kwamba wakiwa na fedha za kutosha basi wataweza kuwa huru watakavyo. Lakini wanakuja kujifunza kwamba hilo siyo kweli, kwa sababu kadiri kipato chao kinavyoongezeka, ndivyo wanavyokosa uhuru zaidi.

Kama tulivyoona nukuu tulizoanza nazo makala hii, mfanyakazi wa kawaida anafanya kazi vizuri kwa masaa 8 kwa siku, anapandishwa cheo na kupata malipo zaidi lakini inambidi afanye kazi masaa 12 kwa siku. Kadhalika anayetoka kwenye ajira ili ajiajiri kupata fedha zaidi anajikuta akifanya kazi muda mrefu zaidi.

Hivyo fedha pekee siyo suluhisho la kuwa na maisha huru, fedha ina mchango mkubwa sana, hilo halina ubishi. Lakini kama unachoangalia ni fedha pekee, unajiandaa kupata matokeo mabovu.

Unahitaji kuwa na mpango sahihi wa kuyafanya maisha yako kuwa huru kama ambavyo tutajifunza kwenye uchambuzi kamili wa kitabu.

SOMA; Uhuru Ni Mtego; Hivi Ndivyo Kila Hatua Tunayopiga Kama Binadamu Inatufanya Kuwa Watumwa Badala Ya Kutupa Uhuru.

TISA; KIPATO MLINGANISHO NI BORA KULIKO KIPATO HALISI.

Kuna watu wawili, John na Mike, John analipwa mshahara wa milioni moja kwa mwezi na Mike analipwa mshahara wa laki tano kwa mwezi, swali ni je nani analipwa zaidi? Jibu liko wazi, John analipwa zaidi ya Mike.

Lakini hatukupata maelezo kamili, iko hivi, John anafanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa mbili usiku (masaa 12 kwa siku) na siku sita za wiki, hivyo kwa wiki anafanya kazi masaa 72. Lakini Mike anafanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa nane mchana (masaa 6 kwa siku) na siku tano za wiki, hivyo kwa wiki anafanya kazi masaa 30. Turudi tena kwenye swali, nani analipwa zaidi?

Kwa kuangalia kipato halisi John analipwa zaidi, lakini kwa kuangalia kipato mlinganisho, John anafanya kazi masaa 72 kwa wiki, sawa na masaa 288 kwa mwezi, na analipwa tsh milioni moja kwa mwezi, hivyo kwa saa anayofanya kazi analipwa tsh 3,500/=. Mike anafanya kazi masaa 30 kwa wiki, hivyo kwa mwezi anafanya kazi masaa 120 na analipwa tsh laki tano, hivyo kwa saa analipwa tsh 4,200/=. Swali ni je nani analipwa zaidi.

Kwa kipato mlinganisho, Mike analipwa zaidi ya John, na hilo liko wazi, japo analipwa mshahara mdogo kuliko John, Mike ana muda mwingi wa kufanya mambo mengine, hivyo ana uhuru zaidi ya John. Hivyo unapofanya maamuzi yako ya kipato, usiangalie tu namba, bali angalia na muda na vingine muhimu.

KUMI; MSONGO MZURI NA MSONGO MBAYA.

Watu hufikiri kwamba msongo ni mbaya na hivyo jukumu letu ni kuhakikisha tunaondokana na kila aina ya msongo kwenye maisha. Lakini hilo siyo kweli, msongo una umuhimu kwenye maisha yetu, ndiyo unatusukuma kuchukua hatua mbalimbali.

Tunachopaswa kujua ni kwamba kuna msongo mzuri na msongo mbaya.

Msongo mbaya ni ule unakufanya kuwa dhaifu, kukuondolea kujiamini na kujifanya ujisikie vibaya. Ukosoaji wenye lengo la kubomoa, kuwa na bosi asiyejali na kujiumiza mwenyewe ni aina ya msongo mbaya ambao unapaswa kuepuka kwenye maisha yako.

Msongo mzuri ni ule ambao unakupa msukumo na hamasa ya kuchukua hatua ili kubadili hali uliyonayo sasa. Kuwa na watu wanaokusukuma upige hatua zaidi, kuchukua hatua za hatari ambazo zinatuwezesha kukua zaidi na kuharakisha kukamilisha jambo kwa wakati ni aina ya msongo mzuri ambao tunapaswa kuutumia kupiga hatua zaidi.

Watu wanaoepuka kila aina ya ukosoaji huwa wanashindwa, lakini wale ambao wanapokea ukosoaji chanya na kuepuka ukosoaji hasi, wanajifunzana kuwa bora zaidi. Hivyo bila ya msongo, mtu huwezi kupiga hatua kubwa.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo sheria kumi unazopaswa kuzijua na kuziishi ili uweze kuwa na uhuru kamili wa maisha yako na kujiunga na kundi la wale ambao wamechagua kuwa na maisha yenye uhuru kwenye muda, fedha na eneo.

Kwenye uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha 4-HOUR WORKWEEK, tunakwenda kujifunza hatua kubwa nne zakuchukua ili kutengeneza uhuru kamili wa maisha yako. Tim Ferris amezipa hatua hizi nne neno DEAL ambapo ni kifupisho cha maneno DEFINE, ELIMINATE, AUTOMATE na LIBARATE. Pia ameonesha jinsi ambavyo waajiriwa wanapaswa kwenye kwa mlolongo wa DELA badala ya DEAL, haya yote tutajifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki. Kupata uchambuzi wa kitabu hiki na vingine vingi, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; https://www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania