Tunapoyaangalia mafanikio ya wengine, huwa tunaona vitu vikubwa sana ambavyo wamevifanya, na hilo linatukatisha tamaa na kuona kwamba hatuwezi kuwafikia.

Kwa mfano wewe unapenda kuwa mwandishi, unamwangalia mtu unayevutiwa kupitia uandishi wake na unakuta ameandika vitabu zaidi ya kumi, tenda ndani ya miaka michache, wewe ukifikiria tu kuandika kitabu kimoja unakata tamaa kabisa.

Ambacho umekuwa huoni ni kwamba yale matokeo unayoyaona kwa nje yanatokana na tabia za msingi ambazo mtu amejijengea ndani yake.

Mfano kwenye uandishi, mwandishi unayeona ameandika vitabu vingi, maana yake huyu amejijengea tabia ya kuandika kila siku. Kila siku kuna kiwango cha maneno ya kuandika amejiwekea, na atafanya hivyo iwe anajisikia au hajisikii. Kwa kuwa na tabia hii, kunamwezesha kutoa kazi nyingi.

Kadhalika kwenye fedha, tunapowaona wale wenye fedha nyingi kuliko sisi tunajiambia hatuwezi kuwafikia. Lakini ambacho hatuoni ni kwamba watu hao hawakuanza wakiwa na fedha kiasi hicho. Badala yake kuna tabia walizojijengea kifedha ambazo zimewafikisha pale walipo sasa. Moja ya tabia hizo ni matumizi kuwa madogo kuliko kipato na kuweka akiba. Wenye tabia hii wanafanya hivyo kwenye kila kipato wanachoingiza na ndiyo inaleta matokeo makubwa.

Wanasema tabia huwa inaanza kidogo kidogo na kwa wepesi, lakini inaporudiwa kwa muda mrefu, madhara yake yanakuwa makubwa sana. Iwe ni tabia nzuri au mbaya, ikishakuwa ndiyo msimamo na kufanywa kila kitu, tabia ina nguvu sana.

Hivyo unapowaangalia wale waliofanikiwa kuliko wewe, unapowaangalia wale ambao ungependa kufika walipofika, usijiambie huwezi kufika au walikofika wao ni mbali, bali jiulize ni tabia zipi walizojijengea na wewe anza kujijengea tabia hizo. Kwa hakika utaweza kunufaika na nguvu ya tabia katika safari yako ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha