“Don’t lament this and don’t get agitated.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.43
Sisi ni nani mpaka tustahili kuiona siku hii ya leo?
Tukiwaangalia wale ambao walikuwa na mipango mikubwa kwa siku hii ila hawajaifikia, ndiyo tunagundua kwamba tuna bahati ya kipekee kuiona siku hii.
Siyo kwa nguvu zetu wala ujanja wetu, bali ni bahati tu.
Hivyo tuitumie bahati hii vizuri kwa kwenda kuweka vizuri vipaumbele vyetu na kuvifanyia kazi.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAMBO YATAKWENDA VIZURI…
Huwa tunakuwa na malengo na mipango mbalimbali.
Huwa tunachukua hatua ili kufikia malengo na mipango hiyo.
Lakini matokeo tunayokuja kuyapata yanakuwa tofauti kabisa na matarajio yetu.
Na hapa ndipo tunapokata tamaa na kuona hatuwezi kupata kile tunachotaka.
Tunalalamika na kulaumu kwa namna ambavyo dunia haiko sawa, na kuamua kutojaribu tena.
Na hapo ndipo tunapojinyima nafasi ya kufanya makubwa zaidi.
Haijalishi umepata matokeo gani sasa, jua kitu hiki kimoja, utakwenda kuwa sawa, mambo yatakwenda vizuri tu huko mbeleni, kama tu utaendelea kuchukua hatua sahihi na kutokukata tamaa.
Hutapata kila unachotaka pale unapojaribu kwa mara ya kwanza, lakini unaporudia kufanya, unajiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo mazuri.
Matokeo unayopata leo siyo matokeo utakayopata kila siku,
Hivyo usikatishwe tamaa na matokeo yoyote unayopata.
Wewe endelea kuchukua hatua sahihi na mambo yako yatakuwa sawa, kuna wakati utafika ambapo matokeo unayoyataka yatakuja.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kwenda kuchukua hatua sahihi na kutokukubali kukatishwa tamaa na matokeo unayoyapata, kwa sababu baadaye utapata matokeo bora zaidi.
#ChukuaHatuaSahihi #PokeaMatokeoNaBoresha #UsilalamikeWalaKukataTamaa
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania