Kwenye juma la 47 la mwaka 2019 tumejifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa STILLNESS IS THE KEY kilichoandikwa na Ryan Holiday. Kupitia kitabu hicho mwandishi ametuonesha jinsi ambavyo nguvu ya utulivu inaweza kutusaidia kuwa na maisha bora sana. Ametupa mbinu za kuweza kujijengea utulivu wa AKILI, ROHO NA MWILI, na hayo yote umepata nafasi ya kujifunza kupitia makala ya TANO ZA JUMA.

Kwenye kitabu hicho, mwandishi ametushirikisha historia fupi ya Winston Churchill na jinsi ambavyo aliweza kutumia nguvu ya utulivu kuweza kuwa na ufanisi na uzalishaji mkubwa sana kipindi cha uongozi wake, na kuwa mtu muhimu sana aliyeisaidia dunia wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.

Kwenye #MAKINIKIA haya, nakwenda kukushirikisha ni jinsi gani Winston Churchill aliweza kuwa na ufanisi huo mkubwa na jinsi wewe pia unaweza kuwa na ufanisi kama wake na ukafanya makubwa.

Karibu sana tujifunze na tuchukue hatua ili maisha yetu yaweze kuwa bora sana.

churchill.jpg

Winston Churchill alikuwa mwanasiasa, mwanajeshi na mwandishi. Alikuwa waziri mkuu wa Uingereza kati ya mwaka 1940 mpaka 1945 ambapo alisaidia kushinda kwenye vita kuu ya pili ya dunia. Pia alikuwa waziri mkuu tena kati ya mwaka 1951 mpaka 1955.

Winston alizaliwa mwaka 1874 na kufariki mwaka 1965, katika kipindi chote cha uhai wake, muda wake mwingi aliutumia kwenye uongozi na uandishi, alipata nafasi za uongozi kwenye ngazi mbalimbali kwa miaka 55 (tangu mwaka 1900 mpaka 1955, akiwa mbunge kwa kipindi chote, waziri kwa miaka 31 na waziri mkuu kwa miaka 9) na pia aliweza kuandika vitabu zaidi ya 40.

Uwezo wa Churchill kufanya yote hayo umekuwa unawashangaza wengi, lakini kupitia maisha yake, tunajifunza jinsi ambavyo nguvu ya utulivu inaweza kutusaidia kufanya makubwa kwenye maisha yetu pia.

Kutoka kwenye kitabu STILLNESS IS THE KEY, mwandishi Ryan Holiday ametushirikisha mambo kumi yaliyomwezesha Churchill kuweza kuwa na ufanisi na uzalishaji mkubwa kuliko mtu mwingine yeyote. Karibu tujifunze mambo haya kumi na tuweze kuyatumia kwenye maisha yetu na kupiga hatua pia.

MOJA; TUNZA NGUVU ZAKO.

Churchill aliwahi kuulizwa swali na mtu, ni kitu gani kimekuwezesha wewe kufanikiwa sana kwenye maisha yako? Bila ya kusita akajibu “kutunza nguvu, kutokusimama wakati unaweza kukaa na kutokukaa wakati unaweza kulala”.

Kwenye jibu hilo moja, tunajifunza kitu kikubwa sana kuhusu ufanisi na uzalishaji, usipoteze muda wako kwa vitu visivyokuwa na umuhimu. Churchill alijua ana majukumu mengi na hivyo aliweka vipaumbele vyake vizuri, kujihusisha na yale ambayo ni muhimu na ya msingi na kuachana na mengine.

Churchill alikuwa mtu wa kuweka malengo makubwa, kutokuruhusu makosa au ukosoaji umrudishe nyuma, kutokupoteza nguvu kwenye majuto au ugomvi na kutenga muda wa kujipa raha. Yote haya yanalenga kutumia vizuri nguvu zake kwa yale yaliyo muhimu zaidi kwake.

Anza sasa kutunza nguvu zako, achana na yale yasiyokuwa na manufaa kwako, weka vipaumbele vyako vizuri na tenga muda wa kujipa raha kwa kufanya hobi yako.

MBILI; NIDHAMU NA MAPENZI.

Kitu kikubwa ambacho kilimwezesha Churchill kufanya makubwa ni kuwa na NIDHAMU NA MAPENZI makubwa kwenye kila alichokuwa anafanya. Hakufanya tu kwa sababu anafanya, bali alifanya kila kitu kwa mapenzi makubwa na kwa lengo la kuacha alama hapa duniani.

Churchill amewahi kunukuliwa akimtania rafiki yake kwa kusema; “sisi wote ni minyoo, viumbe wadogo ambao tunakula, tunakunya na kufa, lakini mimi nataka kuwa mnyoo unaowasha taa”.

Kauli hiyo, japo ni ya utani, lakini imebeba maana kubwa sana kuhusu maisha yetu sisi kama binadamu. Hebu fikiria kama utazaliwa, uishi maisha ya kawaida na kisha kufa, utatofautishwaje na wadudu kama minyoo?

Lakini kama utazaliwa, kuchagua kuishi maisha ya tofauti ambayo yanatoa mchango kwa wengine, utakuwa mnyoo wa tofauti, mnyoo unaotoa mwanga kwa wengine na hivyo kuacha alama ya tofauti.

Jijengee nidhamu na mapenzi kwenye kile unachofanya na usifanye kwa ajili yako, badala yake fanya kwa ajili ya wengine na utaweza kuacha alama hapa duniani.

TATU; VITABU.

Churchill alikuwa mpenzi wa vitabu tangu akiwa mtoto. Alitumia muda mwingi kwenye kusoma vitabu, lakini pia alitumia muda mwingi zaidi kuandika vitabu. Alianza kuandika kama mwandishi wa habari, akiripoti vita ya makaburu Afrika kusini miaka ya 1890, baadaye aliendelea kuandika hata akiwa kiongozi. Ni mtu ambaye aliweza kuiandika historia ya vita ya kwanza ya dunia na vita ya pili ya dunia kwa mapana kuliko mwandishi mwingine yeyote.

Kupitia kusoma vitabu Churchill aliweza kujifunza mambo mengi kuhusu dunia yaliyomsaidia kwenye uongozi na hata uandishi pia. Na kupitia kuandika vitabu alielewa kwa kina yale aliyoyaandika na hivyo yakamsaidia zaidi kwenye uongozi wake.

Jenga ushirika na vitabu, tenga muda wa kujifunza mambo mbalimbali kupitia usomaji wa vitabu. Na yale unayojifunza kupitia usomaji huo, tafuta namna unaweza kuwashirikisha wengine nao wakajifunza, hapo utaelewa zaidi.

NNE; MPANGILIO.

Churchill alipenda sana kuwa na mpangilio wa kila kitu ambacho alikuwa anafanya. Pia alipenda kuwa na maandalizi ya kutosha kwenye chochote kile ambacho alikuwa anakwenda kufanya. Churchill alikuwa akisifika kwa kuwa na majibu mafupi kwa kila aina ya swali, watu wakifikiri ana akili sana, lakini yeye alikiri kwamba alikuwa anafanya maandalizi ya kila aina ili kuweza kukabiliana na kila aina ya hali anayoweza kukutana nayo.

“Kila usiku, huwa nakaa na kutafakari kama kuna kitu cha maana nimekifanya kwenye siku yangu, siyo kila nilichofanya, bali kile cha tofauti na chenye manufaa” alinukuliwa akisema Churchill.

Jijengee tabia ya kuwa na mpangilio kwa kila unachofanya na pia kuwa na maandalizi kabla ya chochote unachofanya. Na muhimu zaidi, jenga utaratibu wa kuihoji kila siku yako na kuona ni kipi chenye manufaa umefanya. Kama hakuna basi siku inayofuata nenda kafanye yale yenye manufaa. Ukiwa mtu wa kujiuliza maswali hayo wewe mwenyewe, utakuwa na ufanisi na uzalishaji mkubwa.

TANO; UTARATIBU WA SIKU.

Tumeona jinsi ambavyo Churchill aliweza kufanya mambo mengi kwenye maisha yake, lakini tunabaki tukijiuliza, aliwezaje yote hayo.

Jibu ni moja, alikuwa na utaratibu ambao alikuwa anaufuata kila siku. Alikuwa na ratiba yake ya kuendesha kila siku yake ambayo aliifuata bila kuivunja.

Ratiba yake ya siku ilikuwa kama ifiatavyo;

  1. Alikuwa akiamka saa mbili asubuhi, na kuoga kwa maji baridi.
  2. Masaa mawili baada ya kuoga alitumia kusoma vitabu.
  3. Baada ya hapo alijibu barua mbalimbali zilizotumwa, hasa zile za kazi zake za uongozi.
  4. Saa sita mchana alikwenda kumsalimia mke wake kwa mara ya kwanza kwenye siku yake. Maisha yake yote aliamini kwamba ili ndoa idumu basi wenza hawapaswi kuonana kabla ya saa sita mchana.
  5. Baada ya hapo alianza kuandika, kulingana na kile alichokuwa anafanyia kazi, kama ni kitabu, hotuba au makala.
  6. Baada ya kuandika alikwenda kupata chakula cha mchana.
  7. Baada ya chakula cha mchana alikwenda kwenye matembezi kwenye shamba lake, huku akilisha samaki na wanyama wengine. Pia alipata nafasi ya kukaa eneo tulivu na kutafakari kwa kina.
  8. Saa tisa alasiri ulikuwa muda wa kulala, alikuwa na utaratibu wa kulala kwa masaa mawili mchana.
  9. Alipoamka ulikuwa ni muda wa kuwa na familia na kupata chakula cha pamoja saa mbili usiku.
  10. Baada ya chakula cha usiku na wengine kwenda kulala, yeye alikwenda tena kuandika kwa angalau masaa mawili kabla ya kulala.

Hii ni ratiba ambayo Churchill aliiweka na kukazana kuifuata kila siku, hata siku za mwisho wa wiki na hata siku za sikukuu.

Tengeneza ratiba ya jinsi utakavyokuwa unaiendesha siku yako, siyo lazima iwe kama ya Churchill, lakini lazima uwe na utaratibu wa unafanya nini na kwa wakati gani, kisha kazana kufuata ratiba hiyo kila siku, itakusaidia kuokoa muda mwingi ambao utaupoteza kama huna ratiba ya siku.

SITA; HOBI.

Kwenye kitabu cha STILLNESS IS THE KEY, tumejifunza umuhimu wa kuwa na hobi, kitu ambacho unafanya kwa sababu unapenda kufanya na hivyo kinakupa raha na nguvu pia.

Churchill aliweza kufanya mengi aliyofanya kwa sababu alikuwa na hobi mbili;

Hobi ya kwanza ilikuwa ni kujenga matofali, alipenda sana kazi ya kujenga matofali na kila siku alijenga angalau matofali mia mbili. Japo kazi hii inatumia nguvu, lakini kwake ilikuwa inampa nguvu zaidi. Mwaka 1927 alimwandikia waziri mkuu barua akimwambia “ nimekuwa na mwezi bora sana, kujenga kibanda na kuandika kitabu, nimeweza kujenga matofali 200 kwa siku na kuandika maneno 2000 kwa siku.”

Hobi ya pili ilikuwa ni uchoraji. Baada ya vita ya kwanza ya dunia, Churchill alijikuta akipata msongo wa mawazo kwa kumbukumbu za vita. Dada yake kwa kuona hilo, alimpa zawadi ya rangi za kuchorea na hapo Churchill alianza uchoraji. Hakuwa mchoraji mzuri lakini aliweza kuchora michoro mingi sana, kwa sababu uchoraji ulimpa utulivu wa hali ya juu.

Churchill aliwahi kunukuliwa akiema “Ili kupata furaha, mtu anapaswa kuwa na angalau hobi mbili au tatu na zote ziwe halisi, zinazokusukuma kufanya kitu halisi.”

Je wewe una hobi? Ni vitu gani unapenda kufanya ambavyo vinakupa raha, vinavyohusisha nguvu na akili lakini hulipwi wala kusifiwa kuvifanya. Tenga muda wa kufanya vitu hivyo kwenye siku yako na vitakupa nguvu ya kufanya makubwa.

SABA; SUBIRA.

Mwaka 1929 Churchill alijikuta kwenye wakati mgumu sana, alitengwa kabisa na siasa kwa kipindi cha miaka 10. Mpaka kufika mwaka 1939 Churchill alikuwa nje kabisa ya uongozi, na yeye alichukulia hilo kama nabii aliyepotelea nyikani.

Katika kipindi hicho, Churchill hakukasirika wala kutaka kulipa visasi, badala yake alikuwa na subira, alijifunza kupitia usomaji wa vitabu, aliandika vitabu, alijenga matofali na kuchora picha mbalimbali. Ulikuwa ni wakati wa mapumziko makubwa kwake ambayo yalimssaidia yeye na taifa lake kushinda vita ya pili ya dunia.

Ni katika kipindi hiki cha kutengwa kisiasa ndipo Churchill alipata muda wa kumsoma Hitler kwa undani na kumwelewa kupitia kitabu chake cha Main Kampf na kugundua jinsi alivyokuwa na nia ovu ya kuitawala dunia.

Churchill aliwahi kunukuliwa akisema “kila nabii kuna wakati analazimishwa kwenda nyikani, ambapo anakaa kwa utulivu, anatafakari na kutahajudi na kurudi akiwa mtu wa tofauti kabisa, mtu mwenye nguvu zaidi.”

Na kweli aliporudi kwenye uongozi mwaka 1939 na kuongoza wakati wa vita ya pili ya dunia, Churchill aliweza kufanya makubwa sana mpaka kuimaliza vita.

NANE; UJASIRI.

Churchil alikuwa jasiri na aliwataka watu wote kuwa jasiri, kupambania kile wanachoamini na kutokukata tamaa.

Siku moja mkwe wake alimuuliza vipi kama Ujerumani itaivamia Uingereza wakati wa vita? Churchill alimjibu “naamini unaweza kupata kisu kutoka jikoni kwako na kukitumia, si ndiyo?” Hapa alimaanisha kwamba kila mtu anapaswa kutumia kile alichonacho katika kupambana. Badala ya kukata tamaa, unapaswa kuangalia kipi unaweza kufanya.

Ipo kauli maarufu sana ambayo Churchill amewahi kuitoa, kauli hiyo ni hii; “Never give in. Never give in. Never, never, never, never—in nothing, great or small, large or petty—never give in, except to convictions of honour and good sense. Never yield to force. Never yield to the apparently overwhelming might of the enemy.” Akimaanisha kawe usikate tamaa, kamwe, kamwe, kamwe, kwa chochote kikubwa au kidogo bali kwa yale yaliyo sahihi. Kamwe usikatishwe tamaa na nguvu ya adui.

Je wewe u aujasiri wa kusimamia kile unachoamini bila ya kukubali kuyumbishwa na yeyote au chochote? Kama huna, jijengee ujasiri huo saa, kwa sababu bila ya ujasiri, huwezi kufanya chochote kikubwa.

TISA; KAZI.

Churchill alikuwa tayari kufanya kazi kuliko mtu mwingine yeyote yule. Tangu Uingereza kutangaza vita dhidi ya Mjerumani mwaka 1939 mpaka mwisho wa vita mwaka 1945, Churchill alikuwa akifanya kazi kila siku na kila saa.

Alikuwa akilala masaa manne pekee kwa siku, kila muda aliokuwa macho ulikuwa muda wa kazi, muda wa mapambano kuhakikisha Uingereza inashinda vita.

Wakati wa vita mke wake alimwandalia mavazi maalumu ambayo aliweza kulala nayo na kuamka moja kwa moja na kwenda kwenye kazi badala ya kupoteza muda kujiandaa. Alikuwa akifanya kazi masaa 110 kwa wiki, wastani wa masaa 16 kwa siku. Alisafiri zaidi ya maili 110,000 kwa miaka mitatu.

Kulikuwa na usemi kwamba wakati wa vita Churchill alikuwa na ratiba ndogo kuliko moto wa msituni na utulivu mdogo kuliko kimbunga. Aliweza kufanya haya yote kwa sababu miaka kumi iliyopita, alikuwa amepumzika, akiwa nje kabisa ya uongozi wa juu.

Kipindi cha vita licha ya kuwa na muda mfupi, bado alijitahidi kupata muda wa kuandika na kuchora, vitu ambavyo vilimwezesha kupata nguvu ya kuendelea zaidi.

Je wewe unaweka kazi kisawasawa kwenye kile ulichochagua kufanyia kazi. Je upo tayari kufanya kazi mara mbili zaidi ya wengine? Kwa sababu iwe upo kwenye biashara au ajira, maisha yako ni vita, kama wewe hupambani, kuna mwenzako anapambana na atakuondoa mara moja.

KUMI; UTANI.

Licha ya kuwa kiongozi makini na aliyefanya makubwa sana, Churchill alijua umuhimu wa utani na hivyo alikuwa akitumia utani pale ilipostahili. Utani huo ulimzuia asipate hasira na kutumia nafasi yake ya uongozi vibaya.

Nancy Astor aliyekuwa mbunge wa kwanza mwanamke nchini Uingereza alikuwa akimkosoa Churchill akiwa waziri mkuu, akisema ni kiongozi mbaya. Kuonesha msisitizo, Nancy alimwambia “kama ungekuwa mume wangu, ningekuwekea sumu kwenye kahawa ufe”, Churchill alimsikiliza kwa makini na kisha kumjibu akisema, “kama wewe ungekuwa ni mke wangu, ningekunywa hiyo kahawa nife”.

Kwa jibu hilo, alichukulia uzito huo wa ukosoaji kama sehemu ya utani na hivyo haikumpa hasira wala kumfanya atumie madaraka yake vibaya. Zipo hakuli nyingi za utani ambazo Churchill alikuwa anazitumia mara kwa mara, kufikisha ujumbe muhimu kwa namna ambayo ni rahisi watu kuelewa.

Tumia utani kupunguza ukali wa chochote unachopitia sasa, jitanie wewe mwenyewe na hata kuchukulia kama utani yale ambayo wengine wanafanya ili kukukasirisha na kukuudhi. Kwa njia hiyo utatunza utulivu wako na kuweza kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi.

Rafiki, tumejifunza kwa kina jinsi ambavyo Winston Churchill alivyoweza kufanya makubwa sana katika uhai wake, na nina imani umeondoka na mambo unayoweza kuyafanyia kazi na wewe ukapiga hatua pia.

Kupata kitabu cha STILLNESS IS THE KEY pamoja na uchambuzi wake wa kina, jiunge na channel ya telegram ya SOMA VITABU TANZANIA. Ingia kwenye telegramu yako na sehemu ya kutafuta andika SOMA VITABU TANZANIA kisha jiunge. Au fungua kiungo hiki; https://www.t.me/somavitabutanzania na bonyeza JOIN kujiunga na channel. Karibu sana tujifunze kupitia vitabu na chambuzi zake.

Uchambuzi huu wa kitabu umeandaliwa na Dr. Makirita Amani.

Dr Makirita ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali. Kuendelea kupata chambuzi hizi za vitabu kwenye TANO ZA JUMA, hakikisha unajiunga na channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram.