“The person who follows reason in all things will have both leisure and a readiness to act—they are at once both cheerful and self-composed.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 10.12b
Hongera mwanamafanikio kwa kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari ONGOZWA NA FIKRA…
Akili zetu ni sawa na gari ambalo lina madereva wawili,
Dereva wa kwanza nu fikra na dereva wa pili ni husia.
Fikra zinatuwezesha kuuona uhalisia na kuwa na sababu sahihi za kufanya kitu.
Hisia zinatuzuia kuuona uhalisia, zinatusukuja kuchukua hatua yoyote ile, iwe ni sahihi au siyo.
Ili kuwa na maisha bora na tulivu, tunapaswa kuendeshwa kwa fikra na siyo kwa hisia.
Tunapaswa kuhakikisha tunafikiri kabla ya kufanya maamuzi na kuchukua hatua.
Pia tunapaswa kutambua kwamba hatuwezi kupata kila tunachotaka kwa wakati ambao tunataka.
Kwa kujua hayo, unakuwa na utulivu na kuweza kutumia vizuri chochote unachokuwa nacho.
Ukiendeshwa na hisia kila wakati utakuwa unasukumwa kuchukua hatua ambazo hazina manufaa yoyote kwako.
Utajikuta umechoka lakini hakuna matokeo bora uliyozalisha.
Kabla ya kufikia maamuzi au kuchukua hatua, jiulize je jambo hili nimepata muda wa kulifikiri au nasukumwa tu na hisia?
Hii itakulazimisha kufikiri kabla ya kufanya chochote kile na hivyo kupunguza makosa unayofanya.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufikiri kwa kina kabla ya kufanya maamuzi na kuchukua hatua, siku ya kuendeshwa na fikra na siyo hisia.
#FikiriKwaUsahihi #KuwaMakiniNaHisia #TumiaVizuriUlichonacho
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania