Rafiki na msomaji wa karibu wa kazi zangu aliwahi kuniuliza swali hili siku moja; Kocha kwa nini huwa huandiki kuhusu mahusiano? Unaandika mambo mengi kuhusu mafanikio, je huoni mahusiano ni muhimu? Nilikubaliana naye kwamba huwa siandiki kuhusu mahusiano, kwa sababu mahusiano ni moja ya mada ambazo kila mtu ana maoni yake, na maoni ya kila mtu yanatofautiana na mtu mwingine, hivyo ni rahisi kuibuka ubishi usio na mantiki wa kila mtu kuamini upande wake ndiyo sahihi.

Leo nakwenda kinyume na utaratibu huo niliojiwekea wa kutokuandika vitu ambavyo watu wanaweka hisia mbele kuliko fikra, na tutakwenda kujadili kwa kina kidogo kuhusu saikolojia ya kuchepuka.

Nakwenda kukushirikisha haya kutoka kwenye kitabu ninachosoma na nitakachokichambua kwa kina kwenye juma hili la 48 la mwaka 2019. Kitabu hicho kinaitwa THE SUBTLE ART OF NOT GIVING A F*CK ambacho kimeandikwa na mwandishi Mark Manson. Kitabu hiki kinatoa ushauri wa mtu kuwa na maisha bora, ambao unapingana na ule ushauri maarufu unaotolewa na wahamasishaji wengi.

subtle art.jpg

Mark Manson anasema wahamasishaji wengi wamekuwa wanatumia HAMASA CHANYA kuwahamasisha watu kuchukua hatua, lakini hilo limekuwa halisaidii. Yeye anakwenda upande mwingine kwa kutumia HAMASA HASI ili kumsukuma mtu kuchukua hatua. Hamasa hasi inaeleza ukweli kuhusu asili yetu sisi binadamu na jinsi ya kwenda na asili hiyo, na siyo kujidanganya. Mfano kwenye udhibiti, hamasa chanya inatuambia tuna nguvu kubwa ya udhibiti ndani yetu na tunaweza kufanya chochote. Lakini hamasa hasi inasema tuna udhibiti mdogo sana wa mambo yanayotokea kwenye maisha yetu, mengi yanatokea kama bahati na siyo juhudi zetu. Inakatisha tamaa eh? Usijali, tutaendelea na mjadala huu kwa kina kwenye makala ya TANO ZA JUMA itakayokuwa na uchambuzi wa kina wa kitabu hicho.

Turudi kwenye mada ya makala ya leo, ambayo ni kuhusu saikolojia ya uchepukaji.

Kwenye kitabu hiki cha THE SUBTLE ART OF NOT GIVING A F*CK Mark anatuambia kiungo muhimu sana kwenye mahusiano yoyote yale, iwe ni ya ndoa, kazi, biashara hata undugu ni uaminifu. Bila ya uaminifu mahusiano yanakosa maana, mtu anaweza kusema anakupenda, anakujali na mengine mengi, lakini kama humwamini, maneno yote hayo yanakosa maana na mahusiano hayawezi kuendelea kuwepo.

Moja ya sababu inayopelekea uaminifu kuvunjika kwenye mahusiano ni kuchepuka kwa mmoja wa walio kwenye mahusiano hayo, na tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanaume ndiyo walio tayari kuchepuka zaidi kuliko wanawake. Na tukirudi kwenye hamasa hasi ambayo Mark ndiyo anaiandikia, inapokuja kwenye mahusiano, wanaume wanapenda zaidi tendo la ndoa huku wanawake wakipenda zaidi kujaliwa.

Mtu aliyepo kwenye mahusiano anapochepuka, yaani kufanya mapenzi nje ya mahusiano yake, siyo kwa sababu ya mahusiano au kwa sababu ya kuvutiwa zaidi na mtu aliyechepuka naye. Bali Mark anasema mtu anayechepuka ni kwa sababu ya maadili yake. Mtu anachepuka pale ambapo maadili na kile anachothamini anakipata kwenye kuchepuka kuliko kwenye mahusiano yake makuu. Pale ambapo mtu anapata kitu anachothamini kuliko mahusiano, anakuwa tayari kuchepuka.

Swali ni je ni vitu gani ambavyo watu wanaweza kuwa wanathamini zaidi kuliko mahusiano yao makuu?

Na majibu ni kuna vitu vingi, kama ambavyo kuna watu wengi.

Mfano wapo watu ambao wanachepuka kutimiza tamaa zao za mwili, kwa sababu wanathamini zaidi tamaa za miili yao kuliko mahusiano.

Wapo watu wanaochepuka ili kuonesha kwamba wana nguvu au mamlaka ya kufanya hivyo. Watu hawa wanathamini zaidi ile hali ya kuwa wanaweza kuwa na yeyote wanayetaka kuliko wanavyothamini mahusiano yao.

Wapo ambao wanachepuka ili kudhibitisha kitu fulani kwao na kwa wengine pia. Labda ni mtu ambaye amekuwa anawasumbua au kuna wenzake ambao wana mahusiano mengi, sasa ili na yeye adhibitishe anaweza, basi anachepuka. Hapa mtu anathamini zaidi kudhibitisha kitu kwa watu kuliko mahusiano yake ya msingi.

Mifano ni mingi na wewe mwenyewe unaweza kuiendeleza hapo, lakini msingi mkuu ni thamani au maadili, unathamini nini zaidi ya nini. Kile ambacho unakipa thamani zaidi ndiyo kinachoshinda unapojikuta njia panda.

VITU VIWILI VINAVYOCHUANA KWENYE THAMANI.

Kwenye mahusiano, kuna vitu viwili ambavyo vinachuana kwenye thamani. Vitu hivi ndiyo vinaamua kama mtu atachepuka au atakuwa mwaminifu kwenye mahusiano yake.

Kitu cha kwanza ni tamaa.

Tamaa ni asili yetu binadamu, huwa tunakuwa na tamaa mbalimbali na hizo ndiyo zinazotusukuma kuchukua hatua mbalimbali kwenye maisha. Tunapenda kula chakula kizuri, kunywa vinywaji vizuri, kulala, kuangalia tamthiliya, kufanya mapenzi, kuperuzi mitandao na mengine mengi. Yote haya tunayafanya kwa sababu ya tamaa ambazo tunazo ndani yetu.

Kitu cha pili ni ukaribu.

Ni asili yetu sisi binadamu kupenda ukaribu na urafiki, kujua kwamba kuna mtu yupo kwa ajili yetu, ambaye amejitoa kweli kwetu na yupo tayari kwa lolote juu yetu. Hiki ndiyo kinachopatikana pale watu wanapofunga ndoa, wanapoambiwa wamekuwa mwili mmoja na kila mmoja ni kwa ajili ya mwenzake.

Sasa kwa bahati mbaya sana, vitu hivi viwili vimekuwa vinakinzana. Ili kupata kimoja, lazima uwe tayari kupoteza kingine, huwezi kupata vyote kwa pamoja. Ili kutimiza tamaa zako, lazima ukose ukaribu na ili kupata ukaribu lazima uwe tayari kutokutimiza tamaa zako.

Sasa hapa ndipo thamani inapohusika na kuchepuka kunapoanza.

Kama mtu anathamini zaidi tamaa zake binafsi kuliko ukaribu wake na mwenza wake, hataweza kujitoa kwa ajili ya mahusiano yake na hivyo ataishia kuchepuka. Na kama mtu anathamini zaidi ule ukaribu alionao na mwenza wake, atakuwa tayari kutokutimiza tamaa za mwili wake na kubaki kuwa mwaminifu kwa mwenza wake.

Kwa namna hii mahusiano yanakuwa kama mizani, upande mmoja tamaa upande mwingine ukaribu, upande unaoelemewa ndiyo upande unaoshinda.

scale-why-people-cheat

Kwa lugha rahisi kabisa, hiyo ndiyo saikolojia ya kuchepuka, ambayo mzizi wake mkuu ni thamani au maadili ambayo mtu anayo. Sababu nyingine za nje ambazo watu wanazielezea ni matokeo tu, mzizi upo kwenye thamani na maadili.

HATUA ZA KUCHUKUA PALE MWENZA WAKO ANAPOCHEPUKA.

Tumeshajifunza saikolojia ya uchepukaji, na kupata mzizi mkuu unaopelekea watu kuchepuka.

Swali ni je unafanya nini pale mwenza wako anapochepuka? Na utaona hapa tunaanza na mwenza ambaye amesalitiwa na siyo kuanza na yule aliyesaliti kwa kuchepuka. Maana mtu anayechepuka hawezi kujisaidia yeye mwenyewe, kwa sababu yeye ndiyo tatizo na siyo rahisi kujiona na kujirekebisha.

Watu wengi wanapokamatwa wakichepuka, huwa wanaomba msamaha na kuahidi kwamba hawatarudia tena, ni shetani tu aliwapitia au hawajui imekuwaje. Wanaweza kuwa wanasema kweli kutoka moyoni, lakini ahadi wanazotoa huwa hazitekelezeki, kwa sababu tatizo lao siyo kuchepuka, bali tatizo ni wanathamini nini, maadili yao ni yapi.

Wachepukaji wengi huona tatizo ni kuchepuka na hivyo wanaweza kulidhibiti, wasichojua ni kwamba tatizo lipo ndani zaidi, tatizo ni wao. Na hivyo wanahitaji msaada mkubwa zaidi ili kuweza kuondoka pale walipo.

Hatua ambayo mchepukaji anapaswa kuchukua ni kuanza kuchimba ndani yake na kujua thamani na maadili yaliyopo ndani yake. Kujua ni kipi anachothamini zaidi, ukaribu au tamaa za mwili. Kuanza kuyaangalia maeneo mengine ya maisha yake na jinsi ambavyo amekuwa wanafanya maamuzi, je amekuwa tayari kukosa kitu kizuri sasa ili kupata kitu bora zaidi baadaye?

Kujitambua binafsi kwa kuchimba thamani zilizopo ndani yako ni sawa na kumenya kitunguu. Kila ganda unalomenya linakupeleka kwenye ganda jipya na kila ganda linakutoa machozi. Unapata picha sasa kwa nini ni vigumu mchepukaji kujirekebisha yeye mwenyewe, kwa sababu hizo zoezi la kuchimba thamani za ndani na ambalo linamtoa mtu machozi siyo rahisi kulifanya mwenyewe. Kwa sababu katika kuchimba huko, inabidi mtu afike mahali na kujiambia “mimi ni mbinafsi, najali zaidi tamaa zangu za mwili kuliko mahusiano, siyaheshimu mahusiano yangu.” Bila mtu kufikia hatua hii ya kukiri thamani yake ambayo ndiyo imevunjika, chochote anachoahidi kuhusu kutokuchepuka hawezi kukitekeleza.

Pale mwenzako anapochepuka na anakuomba msamaha ili muweze kuendelea na mahusiano yenu, kuna vitu viwili unavyoweza kumsaidia kufanya ili atimize hilo.

Kitu cha kwanza ni kumsaidia aweze kujihoji na kutafakari ili kujua thamani na maadili yaliyopo ndani yake, aweze kukiri ni kitu gani ambacho amekuwa anakithamini zaidi na hivyo kumpelekea kufanya maamuzi hayo. Akishajua thamani alizojiwekea ambazo ni mbovu basi anaweza kuweka thamani na maadili sahihi. Kwamba kipaumbele cha kwanza kwake ni mahusiano na vitu vingine vitafuata baada ya hapo.

Kitu cha pili ni kumpa muda wa kutengeneza sifa mpya. Mtu anaweza kuahidi kitu mara moja, lakini kitakachoonesha kweli mtu huyo amedhamiria ni sifa ya muda mrefu. Hivyo unapaswa kumpa mtu muda wa kujenga sifa mpya, muda ambao hatarudi tena kwenye thamani na maadili ya zamani yaliyompelekea kuchepuka. Ni baada ya kumfuatilia mtu kwa muda mrefu na kuangalia maamuzi mbalimbali anayofanya kwenye maisha yake ndiyo unaweza kujiridhisha kama kweli amebadilika.

Zoezi hili linachukua muda mrefu, hivyo linahitaji uvumilivu mkubwa kutoka kwa watu wote wawili ambao wapo kwenye mahusiano.

Mark Manson anamalizia ushauri wake huu kwa kusema uaminifu kwenye mahusiano ni kama sahani ya udongo, ikishavunjika haiwezi kurudi kama mwanzo. Ila ikivunjika mara moja, unaweza kuiunganisha kwa gundi na ikafaa kutumia. Ukiivunja mara ya pili, inaharibika zaidi, lakini kama ukiamua kuiunganisha unaweza kufanikiwa, japo itachukua muda. Lakini kama utaivunja tena na tena na tena, haitafaa kuunganisha tena, maana vipande vitakuwa vingi na huwezi kuviweka pamoja vyote.

Tuboreshe mahusiano yetu kwa kuanza kuchimba thamani ambazo zipo ndani yetu, na tuwasaidie wenzetu nao kuchimba thamani zao ili waepuke kuanguka kwenye usaliti ambao unaishia kuvunja mahusiano mazuri.

Wale wanaochepuka unaweza kuwaangalia kwa nje na kuona ni tamaa zao au makusudi, lakini wengi wanajikuta wameshafanya hivyo bila ya wao kufikiri kwa usahihi. Na hiyo ni kwa sababu msingi wao wa ndani, mfumo wao wa thamani ni mbovu.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 48 ambayo itapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, tutakwenda kujifunza kwa kina jinsi tunavyoweza kuwa na maisha bora kwa kutumia HAMASA HASI, hamasa inayogusa uhalisia wetu sisi binadamu na jinsi ya kuutumia kufanikiwa zaidi. Usikose makala hiyo ya TANO ZA JUMA, jiunge leo na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania

Uchambuzi huu wa kitabu umeandaliwa na Dr. Makirita Amani.

Dr Makirita ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali. Kuendelea kupata chambuzi hizi za vitabu kwenye TANO ZA JUMA, hakikisha unajiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram.

subtle art.jpg