Dunia haijali kuhusu maono na malengo uliyonayo kwenye maisha yake. Dunia inajali mambo yake na wale wanaokuzunguka nao wanajali mambo yao. Wewe peke yako ndiye unayeweza kujali kuhusu maono yako na malengo yako.

Na kwa bahati mbaya sana, wewe mwenyewe kuna wakati unaacha kujali kuhusu maono yako na malengo yako. Unajisahau na kuingia kwenye mitego ya dunia.

Kwa sababu dunia inatumia kila fursa kukutamanisha wewe vitu mbalimbali, vitu ambavyo vitakuondoa kwenye maono na malengo yako na kukuweka ‘bize’ na vitu visivyokuwa na msaada wowote kwako.

Dunia inakutamanisha na habari mpasuko zinazoendelea kila kona ya dunia, ajali iliyotokea mahali fulani na kuua wengi, vita vinavyoendelea, mtu kumuua mwenzake na habari nyingine za aina hiyo.

Dunia inakutamanisha na michezo mbalimbali inayoendelea, mpira wa miguu, ngumi, mpira wa kikapu, riadha na kadhalika. Dunia inakutamanisha sana utumie muda na nguvu zako nyingi kufuatilia michezo hii.

Dunia inakutamanisha na habari za umbea na udaku kuhusu watu maarufu, kila siku hazikosekani skendo mbalimbali kuhusu watu hao, maisha yao binafsi, mahusiano yao, utajiri wao, picha zao za ngono na mengineyo.

Kila kitu ambacho dunia inakuletea na kukuambia ni muhimu lakini hakina mchango kwako kufikia ndoto zako, jua hizo ni njama za dunia kukutoa kwenye maono na malengo yako.

Lazima usimame imara kama kweli unataka kuyafikia malengo na maono makubwa uliyonayo. Lazima ushike udhibiti mkubwa kwa fikra zako na maisha yako kwa ujumla. Lazima uwe tayari kubadilika na kwa yale usiyoweza kubadili basi kwenda nayo kama yalivyo.

Lakini kipaumbele cha kwanza kwako kinapaswa kuwa maono na malengo yako, kinapaswa kuwa hatua unazopiga ili kufika kule unakotaka kufika. Achana kabisa na tamaa za dunia, hazina manufaa yoyote kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha