Matumaini ni mtego ambao umetumika kuwanasa watu wengi sana.
Tunajikuta tunakuwa tegemezi kwa wengine kwa matumaini hewa wanayotupa, ambapo hakuna namna matumaini hayo yanaweza kufikiwa.
Wanasiasa wanatupa matumaini, kwamba tukiwachagua maisha yetu yatakuwa mazuri, kila tunachotaka tunakipata, tunawaamini na kuwategemea. Wanapopata nafasi hadithi yao inabadilika, yale matumaini waliyotupa kwamba watayafanya maisha yetu kuwa mazuri hayatimii, badala yake wanatuambia kuna mambo mengine muhimu zaidi ya kurekebisha. Ukweli tunapopaswa kujua ni kwamba hawawezi kutimiza matumaini waliyoahidi, wanazotoa ni sababu tu, lakini hazina mashiko yoyote.
Dini nazo zinawashikilia watu kwa sababu ya matumaini ambayo zinawapa. Kwamba kama utaamini kwenye dini hiyo, kama utafanya kila unachoambiwa, basi utakwenda mbinguni baada ya kifo chako na maisha yako yote yanakuwa furaha. Lakini watu wanapitia magumu mengi wakiwa hai, ambayo matumaini wanayopewa na dini hayawasaidii kukabiliana na magumu hayo.
Njia ya uhakika ya kuwa na maisha ya hovyo, ni kuweka matumaini ya maisha yako kwa mtu yeyote yule, haijalishi mtu huyo anakuahidi nini. Huwezi kuwa na maisha bora kwa kuweka mategemeo yako kwa mtu mwingine.
Njia pekee ya wewe kuwa na maisha bora, ni kujitegemea wewe mwenyewe. Hapa ndipo unapokuwa na udhibiti kamili wa maisha yako, unapata ukombozi kamili na kuweza kuchukua hatua sahihi za kuyafanya maisha yako kuwa vile unavyotaka yawe.
Na kujitegemea haimaanishi kujitenga na wengine, ni lazima ushirikiane na wengine, lakini siyo kuweka utegemezi wako kwao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,