Kama unataka kufanikiwa, kitu cha kwanza unachopaswa kufanya ni kujitofautisha na watu wengine. Kufanya kile ambacho kila mtu anafanya ni kujiandikisha kwenye darasa la walioshindwa.

Watu wengi wamekuwa wanatumia kujilinganisha na wengine kama njia ya kupiga hatua kwenye maisha yao, wanaangalia wengine wamefanya nini au wamefika wapi na hivyo kuangalia kama nao wamefanya au wamefika.

Kujilinganisha na wengine ni moja ya njia zinazowapelekea wengi kuishia kuwa kama watu wengine, kuwa wa kawaida na kushindwa kujitofautisha.

Hivyo kujilinganisha na wengine ni sumu kwa mafanikio yako.

Lakini kama kujilinganisha huko kutatumiwa kwa usahihi, kunaweza kuwa na manufaa kwako.

Kujilinganisha kunakuwa tatizo pale unapofanya hivyo kwa mapana, mfano unapoyalinganisha maisha yako yote na maisha ya mwingine, lazima utajiona wewe uko nyuma au huna maisha mazuri. Na hata utakapoamua kuchukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa mazuri, utaishia kuwa kama wale unaojilinganisha nao.

Kujilinganisha kunakuwa na manufaa kwako pale unapofanya hivyo kwa wembamba, yaani unachagua eneo dogo sana la kujilinganisha. Mfano kwenye ujuzi wako, ili kukua zaidi, lazima ujifunze kwa watu wengine, hivyo mwanzoni utapima ujuzi wako kwa kujilinganisha na wengine, hasa wale ambao wamekutangulia, na hapo utajifunza maeneo gani unayopaswa kuyaboresha zaidi. Kwa kufanya hivi, utaweza kuboresha zaidi ujuzi ulionao.

Ndiyo hivyo rafiki, kujilinganisha kwa mapana kunakuwa kikwazo kwako kufanikiwa, lakini kujilinganisha kwa wembamba kunakupa fursa ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Tumia kujilinganisha kwa usahihi ili kuwe na manufaa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha