Ipo kauli maarufu kwamba mwekezaji mwenye mafanikio makubwa sana, Warren Buffett ana sheria kuu mbili za uwekezaji.
Sheria ya kwanza ni usipoteze fedha na sheria ya pili ni usisahau sheria ya kwanza. Hivyo tu basi na kwa kufuata sheria hizo mbili ameweza kufanikiwa sana kwenye uwekezaji.
Rafiki, tukiwaangalia watu ambao hawana fedha, ni rahisi kuamini kwamba watu hao hawana fedha kwa sababu hawaingizi kipato cha kutosha au hawana kipato kabisa.
Lakini hilo siyo sahihi, karibu kila mtu kwa zama tunazoishi sasa, ana njia ya kuingiza kipato, hata kama ni kidogo kiasi gani. Hivyo kinachowatofautisha wale wanaokuwa na fedha na wasiokuwa nacho siyo kipato wanachoingiza, bali namba wanavyowekeza kipato hicho.
Wanaokuwa na fedha wanafuata sheria za Buffett na hivyo kuwekeza vizuri fedha zao na hivyo kuzuia zisipotee. Lakini wasiokuwa na fedha hawafuati sheria hiyo, hivyo kinachotokea ni wanapoteza fedha zote walizonazo.
Wale wenye kipato kidogo ndiyo wapo kwenye hatari ya kupoteza zaidi, kwa sababu huwa wanatafuta sana njia za mkato za kuongeza fedha zao kwa haraka. Hivyo wanashawishiwa kuwekeza kwenye sehemu zisizo sahihi na hapo wanapoteza fedha zao zote.
Zielewe na kuziishi sheria kuu mbili za Buffett kwenye fedha, linda sana fedha yako isipotee, weka akiba yako sehemu sahihi ambayo wewe mwenyewe huwezi kuigusa. Lakini pia iwekeze akiba hiyo sehemu sahihi ambapo huwezi kuipoteza.
Nimalizie na kauli ambayo huwa napenda kuitumia kwenye fedha; ‘kila mtu na apende fedha zake’, kama wewe mwenyewe hutapenda fedha zako, hakuna atakayefanya hivyo kwa ajili yako. Mara zote linda fedha zako kwa kuweka akiba na kuwekeza sehemu sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,