Muda na fedha ni rasilimali mbili zenye uhaba mkubwa kwa wengi.

Muulize mtu yeyote ambaye hajapiga hatua fulani ambayo amekuwa anatamani kupiga na atakujibu muda hakuna, fedha hakuna.

Kwa kuangalia maisha ya kawaida, ni rahisi kukubaliana na mtu kwamba hana muda na pia fedha ni changamoto.

Lakini unapoacha kuangalia juu juu na kuingia kumwangalia mtu kiundani, unagundua vitu vya tofauti kabisa.

Unagundua kwamba mtu huyo ana masaa 24 kila siku, kazi yake anaifanya kwa masaa 8 mpaka 10 kwa siku na analala masaa 6 mpaka nane kwa siku. Hivyo ukijumlisha masaa 8 ya kulala na 10 ya kazi, unapata masaa 18. Katika masaa 24 ambayo mtu anayo kwenye siku yake, kuna masaa 6 hayatumii kwenye kazi wala kulala. Lakini hakuna yeyote anayeweza kukuambia huwa anatumia masaa hayo sita kufanya nini kila siku.

Unapoendelea kuangalia kwa undani, unagundua mtu huyo anapata muda wa kula mara tatu kila siku, anapata muda wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kufuatilia maisha ya wengine, ana muda wa kufuatilia habari mbalimbali, ana muda wa kuangalia michezo anayopenda, ana muda wa kubishana na wengine.

Kwa kifupi, mtu huyo ana muda wa kufanya kila kitu ambacho wengine wanafanya, lakini hana muda wa kufanya kile ambacho ni muhimu kwake kupiga hatua. Jambo la kushangaza mno.

Kwenye fedha pia mambo ni hayo hayo. Mtu akikuonesha kipato anachoingiza, akakuorodheshea mahitaji yake, utamwonea huruma. Maana kipato ni kidogo na mahitaji ni mengi.

Lakini pata muda wa kumchunguza mtu huyo kwa undani, kuna vitu utaviona ambavyo hutaamini kama ni mtu huyo uliyemwonea huruma. Utakuta anatoa michango ya sherehe mbalimbali kwa watu wengine, ananunua nguo mpya wakati kuna nguo nyingi anazo hazitumii, utakuta ana utaratibu wa kupata burudani filani mara kwa mara. Na hapa ndipo unapojiuliza fedha hizo anazitoa wapi?

Msimamo wangu siku zote umekuwa ni huu, kila mtu ana muda wa kumtosha na fedha za kutosha kufanya chochote anachotaka kufanya kwenye maisha yake. Kinachowasumbua wengi ni kushindwa kuweka vipaumbele sahihi kwenye yale wanayofanya. Ukiweza kuweka vipaumbele sahihi, muda na fedha kidogo ulizonazo zinakutosha kabisa kupiga hatua kwenye maisha yako.

Kuna muda na fedha ambazo sasa hivi unapoteza kwa mambo yasiyo muhimu, hebu anza kuvitumia vizuri na utaweza kupiga hatua kubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha