“It’s better to conquer grief than to deceive it.”
—SENECA, ON CONSOLATION TO HELVIA, 17.1b
Hongera sana mwanamafanikio kwa kuiona siku hii nyingine nzuri ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIKIMBIE HISIA ZAKO…
Sisi binadamu ni viumbe wa hisia,
Huwa tunadhani tunafanya maamuzi yetu kwa kufikiri, lakini ukweli ni huwa tunayafanya kwa hisia na baadaye kuyahalalisha kwa kufikiri.
Lengo kuu la kujifunza na kuiishi falsafa ni kuhakikisha tunazisimamia vizuri hisia zetu ili zisiwe kikwazo kwetu.
Wengi wamekuwa wanaichukulia falsafa ya ustoa kama falsafa ya watu wasiokuwa na hisia, lakini hakuna mtu wa aina hiyo.
Wote tunahisia, tunachotofautiana ni namna ambavyo tunajibu na kudhibiti hisia zetu.
Moja ya njia ambazo wengi wamekuwa wanajibu hisia zao ni kuzikimbia.
Mtu anapokuwa kwenye hali inayoibua hisia, hasa hasi, anakimbilia kufanya kitu kingine ili kuondokana na hisia hiyo.
Hapa ndipo watu wanatumia vilevi, wanajichanganya na wengine, wanakula, wanaenda kununua vitu na kadhalika.
Ambacho hawaelewi ni kwamba, chochote wanachofanya kukimbia hisia, kinazisogeza mbele hisia hizo na tena kuzikuza zaidi.
Njia pekee bora kwako kujibu hisia ni kuzikabili.
Kuzipokea na kuhakikisha hazikusukumi kufanya chochote kibaya.
Kuziangalia hisia hizo kama mtu wa nje.
Na hapo utaweza kupata utulivu, huku ukiona hisia hizo siyo mbaya kama ulivyokuwa unafikiri.
Pia utajifunza kwamba hisia ni kitu cha kupita lakini wewe unabaki kuwa imara.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukabiliana na hisia zako badala ya kuzikimbia.
#UsikimbieHisia #HisiaZinapita #WeweSiyoHisiaZako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania