“You aren’t bothered, are you, because you weigh a certain amount and not twice as much? So why get worked up that you’ve been given a certain lifespan and not more? Just as you are satisfied with your normal weight, so you should be with the time you’ve been given.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.49

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Na msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kuzingatia maeneo hayo matatu, siku hii ya leo itakuwa bora na ya kipekee saba kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NI NAMBA TU ISIKUSUMBUE…
Kuna namba nyingi ambazo tunazo kwenye maisha yetu lakini hazitusumbui kabisa.
Mfano uzito wa mwili wako ni namba, kama una kilo 60 na mwenzako ana kilo 100, hujioni kama umepunjwa.
Kama mguu wako unavaa kiatu namba 40 na mwenzako anavaa namba 45 hilo halikusumbui hata kidogo.
Au kama urefu wako ni sentimita 160 na mwenzako ana urefu wa sentimita 170 tofauti hiyo haikupi tabu yoyote.

Lakini kuna namba mbili ambazo zinawasumbua sana walio wengi.
Namba hizo ni utajiri na umri wa kuishi.
Kama wewe una utajiri wa bilioni moja na mwenzako ana utajiri wa bilioni 10, utajiona wewe ni masikini kuliko yeye.
Kama utaambiwa unaishi miaka 50 tu na mwenzako ataishi miaka 80, utajiona wewe umepunjwa miaka ya kuishi.
Lakini ukiangalia, hizo ni namba tu, hazibadili maisha yetu kwa namna yoyote ile, bali vile tunavyozichukulia.

Mfano kwa utajiri wako wa bilioni moja, ukiwa na watu wenye utajiri wa milioni 100 wewe ni tajiri mkubwa sana.
Na kwa umri uliopewa wa miaka 50, ukikutana na wake wanaizaliwa na kufa utotoni wewe umeishi miaka mingi mno.
Hivyo rafiki, tunapaswa kujua namba hizi na kutokuruhusu zitusumbue.
Tunapaswa kujua kwamba kilicho muhimu siyo namba, bali namna gani tunatumia namba hizo.
Badala ya kukazana kujilinganisha na wengine kwa namba uliyonayo, kazana kuitumia namba hiyo vizuri.
Kama ambavyo unanunua kiatu cha namba 40 kinachokutosha, badala ya kununua namba 45 ili ulingane na wengine, hivyo pia ndivyo unapaswa kichagua kuishi kwenye muda ulionao na kutumia utajiri wako kufanya yaliyo sahihi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujua kila namba uliyopewa ni yako na kukazana kuiishi badala ya kujilinganisha na namba za wengine.
#IshiKwaNamnaYako #UsiigeMaishaYaWengine #UnaKilaUnachohitaji

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania