Pata picha, umewasha tv kwa ajili ya kuangalia taarifa ya habari za siku nzima. Kisha ikaja habari mpasuko, na ukajiandaa kuiangalia. Mtangazaji akaonekana na kuanza kutangaza, kwamba kwa siku hiyo, kulikuwa na mabasi 20 yaliyotoka Dar kwenda Mbeya na yote yamefika salama kabisa, bila ya tatizo lolote. Utaichukuliaje habari hiyo?
Kwanza utashangaa, kwa sababu hutegemei chombo cha habari kiweke hiyo kama habari mpasuko. Hiyo ni kwa sababu vyombo vya habari huwa havitangazi mambo ya kawaida, bali yale yasiyo ya kawaida. Hivyo kwenye ulimwengu wa habari, kama hakuna kitu kisicho cha kawaida kimetokea basi hakuna habari.
Hivyo ndivyo biashara ya habari ilivyo, japo wengi bado hawajaielewa.
Sasa kibaya sana ni kwamba biashara hii ya habari sasa imeingia kwenye mafanikio pia. Tumekuwa tunapewa hadithi mbalimbali za watu waliofanikiwa. Lakini hadithi zinazopewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari ni zile ambazo kuna kitu kisicho cha kawaida.
Hivyo kila unaposikia hadithi mpya ya mafanikio, unaona kitu kipya unachopaswa kufanya, unaanza kukifanya kabla hujafika mbali unasikia hadithi nyingine, nayo ina kitu kingine cha tofauti.
Hapa ndipo wengi wanapodanganyika na kujikuta wakikimbizana na kila kitu kipya kinachovumishwa kwenye hadithi za mafanikio. Watu wanajikuta kila mara wanajaribu kitu kipya na kushindwa kupata mafanikio.
Rafiki, unapaswa kujua msingi wa mafanikio haubadiliki, ni vitu vile vile unavyopaswa kuvifanya kwa kurudiarudia kwa muda mrefu bila ya kuchoka. Kama unafanya kilicho sahihi, yaani unajua unachotaka, unajua gharama unayopaswa kulipa, unaweka kazi, na una subira na uvumilivu, huna haja ya kuhangaika na hadithi mpya za mafanikio unazosikia kila wakati.
Ielewe biashara ya habari ni kutafuta kitu cha tofauti na kukivumisha, wewe kaa kwenye njia yako na hiyo ndiyo itakayokufikisha wewe kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,