Leo naongea na wale watu ambao walichagua njia fulani, lakini sasa wanafikiria huenda kama wangechukua njia mbadala basi mambo yao yangekuwa rahisi kuliko sasa.

Hawa ni wale watu ambao walikuwa na nafasi ya kuweza kuajiriwa au kujiajiri, wao wakakataa kuajiriwa na kuamua kujiajiri, lakini sasa kwenye kujiajiri wamekutana na magumu na wanafikiria kama wangekubali kuajiriwa huenda mambo yangekuwa mazuri sasa.

Hawa ni wale watu ambao waliamua kuachana na ajira ili kwenda kufanya kile wanachopenda na kukiamini, lakini wamekutana na magumu ambayo hawakutarajia, na wakiwaangalia wale waliowaacha kwenye ajira, mambo yao yanaonekana kuwa mazuri kuliko wao, na hilo linawafanya waone labda walifanya makosa kuondoka kwenye ajira.

Hawa ni wale watu ambao walishauriwa namna fulani na watu wao wa karibu, lakini wao wakaenda kinyume na ushauri wao na kusikiliza mioyo yao, lakini baadaye wamekutana na ugumu na kuanza kufikiria kama wangewasikiliza waliowashauri mambo yao yangekuwa mazuri sasa.

Rafiki, unachopaswa kuelewa ni kwamba hakuna yeyote ambaye mambo yake ni rahisi kuliko wewe. Usidanganywe na tabasamu unazoziona kwenye nyuso za watu au vicheko wanavyovitoa mara kwa mara. Usihadaike na yale wanayoyaonesha kwa nje. Wengi wamechagua kutumia vitu hivyo vya nje kama njia ya kujifariji tu, lakini tambua kila mtu kuna vita kubwa inaendelea ndani yake. Kila mtu kuna magumu anapambana nayo.

Hivyo neno la leo kwako ni hili; umeshaenda mbali sana, huwezi tena kurudi nyuma, umeshaona mengi sana, huwezi kuyaacha yote na kurudi kule unakofikiri ni rahisi zaidi. Kwa hatua ambazo umeshapiga mpaka sasa, na yale ambayo tayari umeshayajua, ukirudi kule unakofikiri ni rahisi kutakuwa kugumu zaidi kwako.

Mfano kama ulishatoka kwenye ajira na kujaribu maisha ya kujiajiri, umeshaonja uhuru wa kutawala muda wako na maisha yako mwenyewe, ukisema urudi tena kwenye ajira sasa, ni kitu kitakachokuwa kigumu sana kwako.

Ugumu wowote unaokutana nao, pambana nao na utafanikiwa. Usikubali hadithi unayojipa kwamba kama ungechukua njia mbadala mambo yako yangekuwa rahisi, hakuna ambaye mambo ni rahisi na mteremko kwake, kila mmoja kuna vita anapambana nayo, pambana na vita yako na waache wengine nao wapambane na zao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha