Mchezaji bora kabisa wa mchezo wa kikapu, akijaribu kucheza mchezo wa mpira wa miguu atashindwa na mtu wa kawaida kabisa kwenye mchezo huo.
Mashindano yoyote unayoingia kwenye eneo ambalo hauko bora, unakwenda kushindwa moja kwa moja, tena na watu ambao hata siyo wabobezi sana.
Leo tunakwenda kuangalia jinsi mashindano ya aina hii yanawapoteza walio wengi kwenye eneo la biashara.
Wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wanaigiza kama vile ni wafanyabiashara wakubwa. Wanawahudumia wateja wa biashara zao kama vile wao ni biashara kubwa. Hapo wanakuwa wamejiingiza kwenye mashindani na biashara kubwa na hilo linawapelekea kushindwa na kupoteza vibaya sana.
Biashara kubwa zina udhaifu mmoja mkubwa, kushindwa kuwa karibu na wateja na hivyo zinajaribu kubadili udhaifu huu kuwa uimara kwa kuwekeza nguvu nyingi kwenye kelele. Kelele hizi zinawapatia wateja wa kutosha kuendesha biashara.
Sasa unashangaa mtu mwenye biashara ndogo na yeye anakaa mbali na wateja wake, anawekeza nguvu nyingi kwenye kelele na kutoa bidhaa au huduma za kawaida kwa watu wa kawaida. Haishangazi kwa nini wengi wanashindwa kukuza biashara zao na kuzidiwa na biashara kubwa.
Uimara wa biashara ndogo upo kwenye ukaribu wake na wateja, hakuna urasimu au ngazi za madaraka katika kutatua changamoto ya mteja. Mteja anaweza kupatiwa kile anachotaka kwa namna anavyotaka yeye. Mteja ni sehemu kuu ya biashara na anapaswa kujiona akiwa sehemu ya biashara hiyo.
Kama upo kwenye biashara ndogo, basi weka muda na nguvu nyingi kwenye huduma ambazo mteja anazipata kwako. Aone kabisa tofauti ya kununua kwako na kwenda kwenye biashara kubwa. Kwa sababu kwako anajisikia kama binadamu, ila kwenye biashara kubwa anajisikia kama kipande kwenye mashine hiyo kubwa.
Usijiingize kwenye mashindano ambayo umeshashindwa kabla hata ya kuanza, badala yake cheza kwenye ubora wako, na hapo ulipo, kuna maeneo mengi ambayo tayari una ubora, yatambue na anza kutoa ubora huo kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,