Moja ya vitu vinavyowazuia watu wengi kupiga hatua kwenye maisha ni kukosa kipimo sahihi cha kujipima na kujifanyia tathmini kwenye maisha yao.

Wengi wanaishi kwa mazoea, leo wakifanya kile walichofanya jana, na kesho kwenda kufanya kile walichofanya leo. Halafu wanaweza kulalamika kwa nini wanajituma sana lakini hawafanikiwi.

Rafiki, ili ufanikiwe, ili upate matokeo ya tofauti, lazima kwanza uanze kuchukua hatua za tofauti.

Na njia ya kujisukuma kuchukua hatua za tofauti ni kujichukulia wewe kama biashara.

Msingi mkuu wa biashara ni huu, kutoa thamani ambayo watu wapo tayari kuilipia. Kama biashara haina thamani ambayo inaitoa, haiwezi kudumu kwa muda mrefu.

Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kuyapima maisha yako, kwa thamani ambayo unaitoa kwa wengine. Kama hakuna thamani unayoitoa, hakuna hatua unazoweza kupiga.

Kama ukiwepo au usipokuwepo hakuna tofauti, ni sawa tu na haupo.

Kama ukiondoka au usipofanya unachofanya hakuna watu wanaokukosa na kukutafuta, hakuna kikubwa unafanya na hutaweza kupiga hatua kubwa.

Kila wakati yatathmini maisha yako kama unavyoitathmini biashara unayotaka kuwekeza au kuinunua. Utaangalia sana ukuaji wa biashara hiyo na wateja iliyonao, pamoja na thamani inayotoa ambapo hakuna biashara nyingine inayotoa.

Kadhalika na kwako pia, kila wakati jipime kama thamani yako inakwenda juu, kama kuna vitu vya tofauti unafanya wengine hawawezi kufanya na kama kuna watu wanakutegemea wewe tu kupitia kile unachofanya.

Jitengeneze wewe kama biashara adimu na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha