Dunia inatupa kila fursa ya kukata kona, kuchukua njia za mkato kwenye kila ambacho tunafanya. Ni rahisi kufanya hivyo kwa sababu kila mtu anafanya hivyo.
Lakini pale unapofanya kitu kisichokuwa sahihi, ni wewe ambaye utabeba matokeo yake na hilo litakusumbua kwa muda mrefu.
Kuepuka usumbufu unaotokana na yale uliyofanya, ni muhimu kuwa mkweli kwako binafsi.
Na ili kuwa mkweli, unapaswa kufanya kile kilicho sahihi na siyo kufanya kile kilicho rahisi. Mfano;
Badala ya kulalamika, chukua hatua.
Badala ya kukosoa, shauri na ongoza.
Badala ya kufuata kundi la wengi, simamia ukweli.
Badala ya kuwa mbinafsi, wahudumie wengine.
Badala ya kufuata njia rahisi, kazana kukua na kuwa na maisha ya tofauti kabisa.
Na pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotarajia, pale unapofanya kilicho sahihi lakini bado matokeo unayopata siyo mazuri, simamia kuwa mkweli kwako, endelea kufanya kilicho sahihi kwa sababu hizi ndizo nyakati ambazo unapikwa kuwa mtu bora zaidi.
Usifuate njia rahisi kwenye maisha, zipo nyingi, badala yake fuata njia inayokufanya kuwa bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,