Upo usemi kwamba dunia siyo mbaya ila walimwengu ndiyo wabaya.

Nasikitika kukufahamisha kwamba usemi huo siyo sahihi. Sehemu ya kwanza kwamba dunia siyo mbaya ni sahihi. Sehemu ya pili ya walimwengu ndiyo wabaya siyo sahihi.

Dunia siyo mbaya na walimwengu siyo wabaya.

Tuanze na dunia siyo mbaya.

Dunia inajiendesha yenyewe, kwa kanuni zake za asili, haijali kama wewe upo au haupo, yenyewe inakwenda kama inavyokwenda. Jua linachomoza na kuzama, mvua zinanyesha, mafuriko yanatokea, matetemeko ya ardhi, vimbunga na mengine mengi.

Yote haya yanatokea siyo kwa sababu wewe upo au unahitaji au kutokuhitaji, ni kwa sababu ya kanuni zinazoiendesha dunia. Hivyo kama kanuni inasema jua liwake na wewe unataka mvua kwa ajili ya mazao yako, utaiona dunia ni mbaya. Lakini hutakuwa sahihi, kwa sababu dunia haijiendeshi kwa matakwa yako wewe.

Dunia haijui hata kama upo, haijui hata ni mipango gani uliyonayo, yenyewe inajiendea tu, hivyo kusema dunia ni mbaya, ni kujisema kwamba hujui jinsi dunia inavyokwenda.

Twende sehemu ya pili, walimwengu siyo wabaya.

Haijalishi watu wamekufanyia nini, jua hili, kwamba walimwengu siyo wabaya.

Kama ilivyo kwa dunia, kila mtu anakazana kupata kile anachotaka, katika kukazana huko, wanaweza kutumia njia ambazo zitakuumiza wewe, lakini hilo haliwafanyi wao kuwa wabaya.

Hakuna mtu mwenye akili zake timamu anayeamka asubuhi na kujiambia leo nakwenda kuyafanya maisha ya watu wengine kuwa magumu. Naenda kuhakikisha kila anayepita barabarani ‘namchomekea’ ili tu kumkera. Hakuna anayeianza siku yake hivyo. Lakini mtu anajikuta amechelewa sehemu aliyokuwa anakwenda, na njia pekee ya kuwahi ni kuanza ‘kuwachomekea’ wengine.

Ukielewa hili kwamba yale watu wanayafanya na yanakuudhi mara nyingi hawafanyi makusudi ili kukuudhi, ila wana sababu fulani za msingi kwao kufanya, utaacha kuwalaumu watu kwa mambo mengi na utaona kweli watu siyo wabaya.

Hivi unafikiri swala akimwona simba anakuja ataanza kujiambia mwenye roho mbaya huyo anakuja? Hapana, swala atakimbia kuokoa maisha yake, maana anajua simba huwa anakula swala, siyo swala la roho mbaya au ubaya, bali ndivyo mambo yalivyo.

Kadhalika kwetu sisi binadamu, tunatofautiana tabia, kuna ambao wakijua kitu wanakisambaza, kuna ambao wakitaka kitu wanaiba, kuna ambao wakiwa na kitu chao ni wachoyo. Wote hawa siyo wabaya, bali ndiyo walivyo. Jukumu lako wewe ni kuzijua tabia hizo za watu na kujiepusha nazo, kama swala anavyojiepusha na simba.

Dunia siyo mbaya, jifunze kuishi kwa misingi yake na walimwengu siyo wabaya, zijue tabia zao na epuka zisiwe na madhara kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha