Chanzo cha nguvu yako ndiyo kitaamua kama utakuwa na maisha ya mafanikio na yenye uhuru au utakuwa na maisha ya kushindwa na yasiyo na uhuru.
Nguvu inaweza kutoka ndani yako na hapa chanzo cha nguvu kinakuwa yale uliyofanya, uwezo na upekee wako na matokeo ambayo unayazalisha kwa wengine na wanayategemea.
Nguvu inaweza kutoka nje na hapa unategemea namna wengine wanavyokuchukulia, kama wanakukubali, kukupenda na kukusifia kwa kile unachofanya.
Kwa zama hizi, watu wamekuwa wanakazana sana na nguvu za nje, ndiyo maana vitu kama mitandao ya kijamii vinapata nguvu sana. Mtu anapima nguvu yake kwa idadi ya marafiki alionao mtandaoni, idadi ya ‘likes’ anazopata kwa picha anazoweka mtandaoni na kadhalika. Kipimo hiki ni dhaifu sana kwa sababu huwezi kukisimamia, mara zote watu wanabadilika na hivyo nguvu hii haiwezi kudumu.
Nguvu sahihi kwako kujenga ni nguvu ya ndani, nguvu inayotokana na mchango unaotoa kwa kile unachofanya. Nguvu hii inachukua muda kujenga, kwa sababu unahitaji muda na utaanza na wachache wanaokuelewa na kunufaika na kile unachofanya. Lakini unakuwa kwenye upande wa nguvu, watu wanakufuata siyo kwa sababu unawaomba au kuwasumbua, bali kwa sababu una kitu chenye manufaa kwao.
Na hapo rafiki yangu, pale watu wanapokazana kuwa na wewe kwa sababu wananufaika, unakuwa umejijengea nguvu kubwa na inayodumu na yenye manufaa kwako pia.
Kazana kujenga nguvu hii kwa kuchagua kutoa thamani kubwa kwa wengine kupitia kile ulichochagua kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,