“Everything lasts for a day, the one who remembers and the remembered.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.35

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kuzingatia maeneo hayo matatu, siku hii ya leo itakuwa bora na ya kipekee sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUHUSU KUKUMBUKWA…
Kuna wakati tunasukumwa kufanya mambo kwa ajili ya kuacha kumbukumbu fulani hapa duniani.
Tukiamini kwa kufanya mambo hayo basi tutakumbukwa milele.
Marcus Aurelius anatuambia kila kitu kinakumbukwa kwa siku moja tu, baada ya hapo kinasahaulika.
Na ukiangalia hili lina ukweli kabisa,
Ukiangalia miaka 10 tu iliyopita, kuna watu waliokuwa maarufu na waliofanya makubwa lakini leo hii hawakumbukwi tena.
Watu wengi wanakumbukwa na wale wanaowazunguka, watu hao wakishaondoka kumbukumbu yao inapotea.

Hili linatukumbusha kuwa wanyenyekevu na wenye utu.
Tukazane kufanya yale yaliyo sahihi na siyo yale ya kutupa umaarufu.
Kwa sababu hakuna umaarufu unaodumu milele, baada ya muda watu watasahau kuhusu wewe au chochote ulichofanya.
Fanya kitu kwa sababu ni sahihi na ndiyo unachokiamini na siyo kwa sababu kitakufanya maarufu au ukumbukwe, kwa sababu kumbukumbu hazidumu muda mrefu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kilicho sahihi na siyo kufanya kitakachokupa umaarufu na kukufanya ukumbukwe. Kumbukumbu zozote kuhusu wewe zitapotea muda mfupi baada ya wewe kuondoka hapa duniani, hivyo zisikusumbue sana.
#KumbukumbuHazidumuMilele #FanyaKilichoSahihi #UsisukumweNaKutakaUmaarufu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania