Changamoto zimekuwa nyingi na kuwasumbua wengi kwa sababu watu wengi kwa sasa ni wepesi mno.
Ni watu ambao hawawezi kuhimili mikiki mikiki ya maisha hasa ile ambayo mtu anapaswa kupitia kama anataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Watu wepesi wana tabia ya kutaka kuwabadili watu wawe kama wanavyotaka wao, wanapojaribu hilo na kushindwa wanakata tamaa na kuona hawawezi kupata watu sahihi kwao. Hii inaanzia kwenye mahusiano, kwenye ushirikiano wa biashara na hata kwenye kuajiri. Watu wepesi hawapo tayari kuwakubali watu jinsi walivyo pamoja na changamoto na madhaifu yao na kuona jinsi gani wanaweza kunufaika nao. Hilo linawasumbua sana.
Watu wepesi hawapendi kupingwa au kukosolewa kwa wanachofikiri au kufanya. Wanaamini kile wanachofikiri au kufanya wao ndiyo sahihi, hasa pale wanapokuwa na cheo au nafasi fulani. Kwa njia hii watu hawa hawajifunzi, wanajifungia na uelewa wao mdogo na hivyo wanazidi kuwa wepesi. Watu wepesi wanataka kila mtu akubaliane nao kwenye kile wanachofikiri au kufanya, na inapotokea baadhi hawakubaliani nao, wanaona watu hao wana matatizo au kukata tamaa na kutokufanya wanachotaka kufanya.
Kama umejiona una viashiria au tabia za watu wepesi, ni wakati wa kubadilika, ondoka kwenye wepesi na nenda kwenye ugumu.
Wakubali watu jinsi walivyo na kisha ona ni kwa namna gani unaweza kunufaika nao.
Kubali kukosolewa au kupingwa na wengine, jifunze kupitia mtazamo wa tofauti ambao watu hao wanao.
Karibisha changamoto mbalimbali badala ya kuzikimbia, maana hizo zinakufanya kuwa imara zaidi.
Maisha ni vile unavyochagua kuyaishi, chagua kuwa mgumu na siyo mwepesi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha , nachagua kuwa mgumu kuanzia sasa na kuendelea .
LikeLike
Vizuri sana.
Kila la kheri.
LikeLike