Kikwazo kingine kwenye mafanikio ya wengi ni kufikiri wakishafikia lengo fulani au kupata kitu fulani ndiyo watakuwa na furaha. Ukweli ni kwamba mambo huwa hayaendi hivyo, kama unafanya kitu kwa lengo la kupata furaha utakapokamilisha, ni njia ya uhakika ya kujikosesha furaha.
Badala yake unapaswa kuanza na furaha, furaha inapaswa kuwepo wakati wa kufanya na siyo kusubiri mpaka utakapomaliza au utakapopata unachotaka. Kwa sababu kufanya kunachukua muda, na matokeo ni ya muda mfupi tu.
Leo hii, orodhesha vitu vyote ambavyo vinakupa furaha, kisha fanya vitu hivyo zaidi kuliko vitu vingine. Na elewa vizuri hapa, viti viwe vinakupa furaha na siyo raha. Usije ukasema kuangalia tv kunakupa furaha, hiyo siyo furaha, bali ni raha. Furaha ni pale unapofanya kitu unachopenda na ambacho kina mchango kwa wengine, kinafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.
Kila mmoja wetu ana vitu vya aina hii, vitu ambavyo anapata msukumo mkubwa wa kuvifanya na yupo tayari kufanya hata kama hakuna anayemsifia au kumlipa. Hivi ndivyo vitu ambavyo vina mafanikio yako, vifanye kwa wingi.
Furaha haipo mwisho wa safari, bali furaha ndiyo safari yenyewe. Usiahirishe furaha mpaka utakapofika mwisho, bali anza na furaha kwenye kile unachofanya sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,