Wote tunajua hili, kwamba dini ya kweli ni upendo, kwamba njia pekee ya kufanikiwa ni kuwa mtu wa upendo.
Lakini neno upendo limekuwa linatumika vibaya, na kuishia kuzalisha uzembe badala ya kuzalisha matokeo mazuri.
Watu wengi hufikiri upendo ni huruma na kutowaadhibu au kuwawajibisha watu. Hilo siyo sahihi, na limekuwa linafanya wengi kupotea kwa kigezo cha upendo.
Tuchukue mfano wa watoto, unawapenda watoto wako, lakini pale wanapokosea unawaadhibu. Unawapa adhabu siyo kwa sababu huwapendi au unataka kuwatesa, bali kwa sababu unawapenda na adhabu hiyo itawasaidia kuwa bora zaidi baadaye.
Sasa huo ndiyo aina sahihi ya upendo ambao unapaswa kuwa nao kwenye maisha yako, kwako mwenyewe na kwa wengine pia. Upendo wenye kuwajibika na kukazana kuwa bora kwa njia zilizo sahihi, hata kama zina maumivu.
Upendo wa kweli siyo kuogopa kumwambia mtu ukweli ambao utamuumiza, badala yake kumweleza mtu ukweli jinsi ulivyo na hata akiumia, anakuwa ameujua ukweli na hivyo kuchukua hatua sahihi ili kuwa bora zaidi.
Upendo wa kweli ni kuwa tayari kumwadhibu, kumwajibisha na hata kumsimamia mtu unayempanda kweli, bila ya kuruhusu hisia zikuzuie. Lazima uwe imara sana kwenye hili, kwa sababu hisia huwa ni kikwazo cha kwanza kwetu katika kuishi uhalisia wetu.
Upendo wa kweli ni kuishi ukweli wako na kisha kuwatafuta wale ambao wanaweza kwenda na wewe kwa ukweli unaoishi, na siyo kuishi maigizo ili tu kukubalika na watu fulani.
Upendo wa kweli ni mgumu a unahitaji mtu uwe mgumu kweli.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,