Moja ya vitu vinavyokuzuia wewe kufanikiwa ni jamii inayokuzunguka.

Jamii hiyo imeshakutengenezea boksi na kukuweka kwenye boksi hilo.

Kila unapojaribu kutoka kwenye boksi hilo, jamii inakuzuia, kwa kukutisha na kukukatisha tamaa.

Hivyo umeendelea kukaa kwenye boksi hilo, ukiamini ndiyo kitu salama kwako, lakini ukweli ni kwamba unajizuia kufanikiwa.

unachain.jpg

Jamii imekuweka kwenye boksi kwamba wewe ni mwajiriwa na huwezi kuwa na maisha nje ya ajira yako, hivyo kukushawishi uendelee na ajira yako, hata kama huipendi au haikulipi vizuri.

Jamii imekuweka kwenye boksi kwamba wewe ni msomi, una elimu kubwa na ya juu hivyo unapaswa kujihusisha na vitu vya hadhi yako tu. Hilo linakuzuia wewe kufanya vitu ambavyo vinaonekana ni vya chini ya hadhi yako, hata kama ndiyo unavipenda na vina manufaa kwako.

Jamii imekuweka kwenye boksi kwamba wewe ni masikini, na chochote utakachofanya utarudi kwenye umasikini wako. Hivyo kila kipato unachopata jamii inakushawishi utumie chote, na ukimaliza inakushawishi ukakope. Yote hiyo ni kuhakikisha hutoki kwenye boksi ambalo jamii imekuweka.

Jamii imekuweka kwenye boksi kwamba wewe ni mtu wa kushindwa, ulifeli shule, ukajaribu biashara ikashindwa, ukatapa kazi ukafukuzwa, hivyo kila wakati jamii inakukumbusha wewe ni mtu wa kushindwa, na unapojaribu kitu kipya unaishia kushindwa.

Rafiki, jamii inayokuzunguka ndiyo kikwazo cha kwanza cha mafanikio kwenye maisha yako, kwa mifano uliyoona hapo juu na mingine mengi ambayo unaendelea kuifikiria, unapata picha kwa nini mambo yamekuwa magumu kwako kwa muda mrefu.

Sasa leo tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kupata uhuru wako kutoka kwenye vifungo hivi vya kijamii, ili uweze kuwa na maisha bora kwako na yenye mafanikio makubwa.

Aliyekuwa mwandishi na mwanafalsafa Ralph Waldo Emarson kwenye insha yake aliyoiita SELF-RELIANCE ametushirikisha njia bora sana ya kuchagua kuyaishi maisha yako, kuweza kujiamini na KUJITEGEMEA.

Anasema unapaswa kuandaa hotuba au ujumbe ufuatao na kuwapa wale wote wanaokuzunguka, bila ya hofu wala wasiwasi;

‘Kwako mtu wangu wa karibu, (baba, mama, kaka, rafiki…)

Nimeishi na wewe tangu nazaliwa mpaka hapa nilipofika sasa.

Lakini kuanzia sasa na siku zijazo, nakwenda kuuishi ukweli kwenye maisha yako.

Napenda utambue kwamba kuanzia sasa sitafuata sheria au utaratibu wowote ambao siyo sahihi. Sitakuwa na maagano na mtu yeyote bali nitakuwa na undugu na kila mtu.

Nitakazana kujenga mahusiano bora na kila aliye wa karibu kwangu, lakini mahusiano hayo yatajengwa kwa msingi mpya. Sitafungwa na mila au taratibu zisizokuwa na manufaa.

Mara zote nitakazana kuwa mimi, kujiamini na kujithamini pamoja na kufanya kilicho sahihi. Sitajiumiza kwa ajili ya mtu yeyote.

Kama utaweza kunipanda kwa jinsi nilivyo basi tutafurahi pamoja. Kama huwezi bado nitakupenda.

Sitaficha ninachopenda au nisichopenda, nitakueleza wazi. Nitafanya kilicho sahihi kwangu na kile ambacho nafurahia na kuridhika kukifanya.

Kama utakuwa mtu safi nitakupenda, kama hutakuwa mtu safi sitakuumiza. Kama hutakuwa mkweli basi tafuta watu wengine wa kwenda nao.

Nafanya haya yote siyo kwa sababu ya ubinafsi bali kwa unyenyekevu na ukweli. Kwa sababu ni kwa manufaa ya kila mmoja wetu kuweza kuyaishi maisha halisi kwake na siyo kuigiza maisha ya wengine.

Maamuzi haya yanaweza kuonekana ni ya kikatili, lakini ni yenye manufaa kwangu na kwako, kwa sababu nikiweza kuishi ukweli wangu na wewe ukaweza kuishi ukweli wako, tutakuwa na mahusiano bora zaidi.’

Rafiki, huo ndiyo ujumbe ambao unapaswa kutoa kwa wale wote wanaokuzunguka, ili uweze kupata uhuru wako. Ili kila mtu aweze kujua unasimamia wapi na aweze kukuheshimu kwa msimamo wako.

Halitakuwa jambo rahisi, haitakuwa hatua rahisi kwako kuchukua, jamii itaendelea kuhakikisha unabaki kwenye boksi ambalo imekuweka, hivyo lazima uwe tayari kusimamia kile unachoamini.

Kwenye insha hii ya kujitegemea, Emerson amefundisha mambo mengine muhimu, ya jinsi ya kuchagua kuwa na maisha yako na kufikia ukuu. Kwenye CHANNEL YA SOMA VITABU TANZANIA, uchambuzi kamili wa insha hiyo umewekwa ambao una mambo 25 ya kujifunza na kufanyia kazi ili uweze kuishi maisha yako na kujitegemea. Karibu ujiunge na channel hiyo ili kupata uchambuzi huo na wa vitabu vingine. Kujiunga na channel fungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania