“If you wish to improve, be content to be seen as ignorant or clueless about some things.” – Epictetus
Ni bahati iliyoje kwetu sisi kuweza kuiona siku hii mpya ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha yako, kubali kuonekana mjinga kwenye baadhi ya mambo.
Tunaishi kwenye zama ambazo mambo ni mengi na muda ni mchache,
Hivyo ukitaka kuhangaika na kila linalokuja mbele yako, huwezi kupiga hatua.
Ukitaka kujua kila kinachoendelea hutapata muda na nguvu za kufanya yale muhimu kwako.
Ndiyo maana Epictetus anatuambia kama tunataka kufanikiwa, lazima tuwe tayari kuonekana wajinga kwenye baadhi ya mambo.
Anachotuambia ni kwamba tunapaswa kuchagua kile tunachotaka kupiga hatua, kisha kujihusisha na hicho tu, na mengine yote kuyapuuza.
Usijisikie vibaya pale unapokua hujui ni nini kinaendelea kwenye mambo mengine, muhimu ni kujua kila kinachoendelea kwenye kile ulichochagua.
Ukipelekea rasilimali zako zote (muda, nguvu, umakini) kwenye eneo moja au machache, utapata matokeo makubwa kuliko kuhangaika na kila kitu kinachokuja mbele yako.
Usione kama unapitwa, bali chagua kipi muhimu kwako na mengine achana nayo.
Chagua ni biashara au kazi gani unataka kufanikiwa kupitia hiyo, na kisha puuza nyingone zote.
Akija mtu na kukuambia kuna fursa bora sana ya kibiashara, kama haiendani na kile ulichochagua kufanya, achana nayo mara moja na rudi kwenye eneo lako.
Huna muda wala nguvu au umakini wa kuweza kuhangaika na kila kitu.
Chagua vitu vichache utakavyohangaika navyo na kisha puuza vingine vyote.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania