“We should be ready to change our views at any time, and slough off prejudices, and live with an open and receptive mind. A sailor who sets the same sails all the time, without making changes when the wind changes, will never reach his harbor.” —HENRY GEORGE
Ni jambo la kushukuru sana kwa sisi kuweza kuiona siku hii nyingine nzuri sama ya leo.
Tunapaswa kuitumia siku hii kufanya mambo makubwa na ya kipekee na siyo kuipoteza kwa kufanya yale yasiyo na tija.
Kwenye maisha, unapaswa kuwa tayari kubadili mtazamo wako kulingana na mambo yanavyobadilika.
Unapaswa kuachana na upendeleo ulionao na kuishi kwa fikra zilizo wazi na zinazoweza kupokea mabadiliko mbalimbali.
Baharia anayeweka tanga lake kwa namna moja bila ya kubadili kulingana na upepo unavyobadilika hawezi kufika kwenye bandari anayokusudia kufika.
Kadhalika wewe kuendelea na mipango yako kama ilivyokuwa licha ya mambo kubadilika huwezi kuyafikia malengo yako.
Tunaposema uwe tayari kubadilika, hatumaanishi kila wakati ubadili maono uliyonayo au malengo uliyojiwekea.
Badala yake unapaswa kubadili njia unazotumia kufikia maono na malengo yako kama kuna mambo yamebadilika ambayo yanazifanya njia unazotumia sasa zisikufikishe kwenye maono na malengo yako.
Kadhalika pia kwenye mtazamo ambao mtu unakuwa nao, mambo yanapobadilika mtazamo wako unaweza kuwa kikwazo kwako. Hivyo unapaswa kubadili mtazamo wako ili uweze kuendana na hali ya mambo.
Siku hii ikawe siku ya kupima kila mpango ulionao wa kufikia maono na malengo uliyonayo na kisha kujiuliza kama njia hiyo ni sahihi au inahitaji mabadiliko.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania