“How long are you going to wait before you demand the best of yourself.” – Epictetus

Unasubiri mpaka lini ndiyo uanze kujidai na kujisukuma kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako?
Kwa sababu hapo ulipo, kuna uwezo mkubwa sana unao, lakini cha kushangaza huutumii.
Na wengi wamekuwa wanakufa na uwezo huo, bila ya kuutumia kwa sababu hawajikamati na kujisimamia kuhakikisha wanatumia uwezo wao, kwa sababu wengi pia hawajui kama wana uwezo mkubwa ndani yao.

Wachache wamekuwa wanaamshwa usingizini na matukio ambayo yanabadili kabisa maisha yao,
Mfano mtu anafukuzwa kazi na hapo ndipo anagundua kwamba anaweza kujiajiri mwenyewe na akafanya makubwa.
Au mtu ananusurika kwenye ajali mbaya ambayo wengine wamekufa na hapo ndiyo anajua kwamba amekuwa anapoteza maisha yake na hivyo kuanza kuyapa umakini.
Wengine ni hasira za kukataliwa au kudharauliwa ndiyo zinawasukuma kufanya makubwa.

Sasa wewe huna haja ya kusubiri mpaka majanga ya aina hiyo yakukute, badala yake unapaswa kuanza sasa.
Nimeshakuambia na umeshajua kwamba kwa chochote unachofanya sasa, unao uwezo wa kufanya zaidi, yaani kwa kiwango cha chini kabisa, unaweza kufanya mara mbili ya unavyofanya sasa.

Swali ni unasubiri nini na utasubiri mpaka lini?
Kwa sababu umeshajua uwezo unao na muda pekee ulionao ni sasa, basi anza kuchukua hatua.
Kataa kuwa kawaida, kataa kupoteza uwezo ulio ndani yako na anza kujisimamia na kujidai ule uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Ukawe na wakati mwema, kabla hujalala andika kipi cha tofauti unakwenda kufanya kesho na unapoianza kesho anza na hicho.

Kocha.