Kila mtu kuna wakati huwa anajikuta njia panda, anakosa uhakika wa kitu gani afanye.
Unajikuta una machaguo mengi na hujui kipi ni sahihi kwako kufanya.
Huu ndiyo wakati ambapo wengi hupoteza muda wakifikiria kipi sahihi kwao kufanya.
Wengi hukimbilia kujifunza zaidi, kufanya tafiti zaidi, kuomba ushauri kwa wengi zaidi.
Lakini hatua hizo badala ya kuwapeleka mbele, zinazidi kuwakwamisha. Hivyo wanazidi kupata taarifa nyingi ambazo zinawaweka njia panda zaidi.
Leo nataka kukupa njia rahisi ya kukuondoa kwenye mkwamo unaokutana nao pale unapokosa uhakika.
Njia hiyo ni kufanya tathmini ya mkwamo huo na matokeo mabaya kabisa unayoweza kupata kwa kuchagua njia yoyote. Je nini kibaya zaidi kinaweza kutokea? Je utakufa? Je utapoteza kila kitu?
Ukijiuliza maswali hayo, utagundua ni mara chache sana ambapo matokeo utakayoyapata ni mabaya na yenye madhara makubwa. Lakini mara nyingi matokeo, japo siyo mazuri, lakini hayawi ya kutisha.
Baada ya kujua hili, chagua kuchukua hatua yoyote kati ya zile zilizokuweka njia panda.
Ndiyo, acha kuchambua kila hatua na anza na moja wapo, ifanyie kazi na matokeo utakayoyapata yatakupa nafasi ya kuboresha zaidi. Kwa kufanya, unajifunza zaidi kuliko kuchambua.
Ni bora ukosee kwa kufanya kuliko uwe sahihi kwa kuchambua.
Hivyo chagua kufanya chochote na anza kuchukua hatua. Na kama bado hujui utachaguaje, tumia njia holela, rusha shilingi au funga macho na kuchagua.
Muhimu ni ufanye kitu, mengine yatajipanga yenyewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,