Huwezi kwenda kwenye shamba, ukapanda mbegu halafu ukaondoka na kusubiri kuja kuvuna. Asili haifanyi kazi hivyo, ni lazima ufanye uwekezaji mkubwa kwenye shamba hilo kama unataka kupata mazao mengi na mazuri.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio yako, huwezi kusema unataka kufanikiwa, ukajiwekea maono na malengo yako ya mafanikio halafu ukasubiri kufikia mafanikio hayo. Ingekuwa rahisi hivyo kila mtu angekuwa amefanikiwa sana.
Unapaswa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mafanikio yako. Baada ya kujua nini hasa unachotaka, baada ya kujua wapi unataka kufika, kinachofuata ni uwekezaji mkubwa wa nguvu, akili, fedha, muda na hisia ili kuweza kufika hapo.
Nguvu unahitaji kujitoa kweli kuweka kazi ili kufika kule unakotaka kufika, kazi kwako wewe mwenyewe kwa kujua ubora wako na madhaifu yako, na kazi kwenye kile unachofanyia kazi.
Akili ni lazima uinoe sana ili iweze kufanya maamuzi sahihi kwako, lazima ujifunze kupitia njia mbalimbali ili kuiweka akili yako kwenye hali bora ya kufanya maamuzi.
Fedha zitahitajika sana, kuanzia kwenye kujinoa wewe mwenyewe mpaka kwenye kuwekeza kwenye kile unachofanya. Kuna wakati utaweka fedha eneo fulani ukitegemea kupata faida ukaishia kupata hasara, hiyo ni sehemu ya uwekezaji kwenye mafanikio yako kwa sababu unaondoka na somo muhimu.
Muda ndiyo uwekezaji unaopaswa kuwa tayari kuuweka, wengi wamekuwa wanafikiria kuna njia ya mkato ya kufanikiwa, kulala masikini na kuamka tajiri. Njia hiyo haijawahi kuwepo, haipo na haitakuja kuwepo. Kama umejiambia unataka kufikia mafanikio makubwa, basi muda mfupi kwako ni miaka kumi, na kwa sehemu kubwa itakuwa zaidi ya hapo.
Hisia ndiyo zitakazokuvusha kwenye nyakati ngumu, safari yako ya mafanikio itakuwa na vikwazo vya kila aina, vikwazo ambavyo vinakatisha tamaa. Kitu pekee kitakachokuvusha kwenye vikwazo hizi ni mtazamo chanya na hisia chanya unazokuwa nazo, kuwa na matumaini kwamba licha ya yote unayopitia, mbele kuna mwanga mkubwa.
Rafiki, kama haupo tayari kuwekeza vitu hivi, ni bora usijidanganye kwamba utafanikiwa, maana utaishia kujiumiza. Unaposema unataka kufanikiwa, lazima uoneshe hilo kweli, lazima ufanye uwekezaji sahihi kwa mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana kocha, nimependa hili, muda mfupi kwangu ni ili kufanikiwa katika maisha ni miaka kumi na mara nyingi itakuwa zaidi ya hiyo.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike