“We live a senseless life, contrary to the understanding of life by the wisest people of all times. This happens because our young generations are educated in the wrong way—they are taught different sciences but they are not taught the meaning of life.” – Leo Tolstoy
Kuiona siku hii nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu na nafasi bora sana kwetu.
Tunapaswa kuitumia nafasi na siku hii vizuri ili iweze kuwa na tija kwetu na kwa wengine pia.
Tumekuwa tunapata elimu nyingi kwa njia mbalimbali,
Kuanzia shuleni ambapo tumetumia miaka mingi kufundishwa kila aina ya sayansi na sanaa.
Na pia kwenye maisha yetu ya kawaida ambapo tunajifunza kwa njia mbalimbali, ikiwepo kujisomea au kutoka kwa wengine.
Lakini pamoja na elimu zote tunazopata, kuna elimu moja muhimu sana ambayo unaikosa.
Elimu hiyo ni kuhusu MAANA YA MAISHA.
Tunayaishi maisha yetu kila siku, lakini hayujawahi kukaa chini na kujifunza au kufundishwa maana ya maisha yetu hapa duniani.
Tunajifunza mpaka maisha ya wanyama na wadudu, lakini kuhusu maisha yetu wenyewe, ambayo ndiyo tunayaishi kila siku, tunakosa kabisa uelewa wa msingi.
Kutokujua maana ya maisha kumefanya wengi kuwa na maisha mabovu, maisha yaliyojaa msongo na ya kuwasindikiza tu wengine.
Kutokujua maana ya maisha kumefanya wengi kuhangaika na maisha ya wengine, kuiga kile ambacho wengine wanafanya hata kama hakina maana kwao.
Waliotutangulia, licha ya kwamba walikosa elimu bora kama tunayopata sasa, walipata elimu hii ya msingi kabisa, kuhusu maana ya maisha.
Na hiyo iliwapelekea kuwa na maisha yenye utulivu huku wakijihusisha na yale yaliyo muhimu kwao na kupuuza yasiyo muhimu.
Kwa kuwa hakuna ambaye yupo tayari kukufundisha kuhusu maana ya maisha, basi hili ni jukumu ambalo unapaswa kulibeba wewe mwenyewe.
Jifunze na ujue maana ya maisha yako,
Jua kwa nini uko hapa duniani,
Jua kusudi la wewe kuwa hapa,
Kisha liishi kusudi hilo kila siku,
Uhangaike na yale muhimu kwako huku ukipuuza yasiyo muhimu.
Ukijua maana ya maisha yako, maisha yanakuwa tulivu na unayoyafutahia hata kama unapitia magumu kiasi gani, kwa sababu unaijua maana.
Usikubali kuendelea na maisha bila ya kujua maana yake kwako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania