Wale wanaotaka kukutawala, kukuhadaa, kukushawishi au kukutapeli, wanajua sehemu sahihi ya kushika. Sehemu hiyo ni fikra zako. Mtu yeyote akishaweza kuzishika fikra zako na ukakubaliana naye, basi utakubali kila anachokuambua, hata kama siyo sahihi kwako.

Fikra zetu zina nguvu kubwa sana kwenye maisha yetu. Na kama wanafalsafa wengi walivyowahi kusema, unakuwa kile unachofikiri, hivyo unapaswa kuwa makini sana na fikra unazoruhusu ziingie kwenye akili yako.

Leo nakwenda kukushirikisha nguvu nyingine ya fikra zetu, hasa upande wa nidhamu.

Watu wengi sana wanajua nini wanataka kwenye maisha yao, na wengi wa hao wanajua nini wanapaswa kufanya ili kupata wanachotaka. Lakini cha kushangaza, ni wachache sana ambao wanafanya na kupata wanachotaka.

Nini kinawakumba wengi wanaojua wanachotaka na kile wanachopaswa kufanya ili kupata lakini hawapati? Jibu ni moja, wanakosa nidhamu.

Kila mtu ambaye amewahi kujaribu kupunguza uzito anajua kabisa nini anapaswa kufanya ili apunguze uzito wake, lakini hafanyi na hivyo uzito haupungui.

Kila aliye na changamoto za kifedha anajua kabisa nini anapaswa kufanya ili kuondoka kwenye changamoto hizo, lakini hafanyi.

Nidhamu ni kikwazo kikubwa ambacho kinawazuia wengi kupiga hatua kwenye maisha yao.

Wengi wamekuwa wanajiuliza ni jinsi gani wanaweza kujijengea nidhamu, ni kwa namna gani wataweza kujisukuma kufanya kile wanachopanga kufanya bila ya kuahirisha, kuacha au kukata tamaa.

Na jibu ni hili, anza kwa kudhibiti fikra zako. Nidhamu inaanza pale unapoweza kudhibiti fikra zako, kwa sababu ukiweza kudhibiti unavyofikiri, basi pia utaweza kudhibiti unachofanya.

Watu wengi wanashindwa kufanya wanachofanya, kwa sababu fikra zako ziko tofauti na kile wanachotaka kufanya. Wengi wanaona wanachofanya ni kama adhabu, kitu ambacho ni tofauti kabisa na wao.

Lakini fikra sahihi unazopaswa kuwa nazo ni kujiona tayari umeshakuwa au umeshapata kile unachotaka, na kufanya kwako ni sehemu ya wewe kuwa na kitu hicho.

Yaani kama lengo lako ni kupunguza uzito, unapochukua hatua usijione kama mtu ambaye ana uzito uliopitiliza na anataka kuupunguza, badala yake jione kama mtu ambaye tayari ameshapungua uzito hivyo hataki uongezeke tena.

Sijui umeona namna kubadili fikra kunavyokubadili wewe na hatua unazochukua. Ukishajiona kwamba umeshapungua uzito, hakuna kushindwa, hivyo huwezi kuishia njiani, unajiona kila unachofanya ni sehemu ya maisha yako.

Hatua ya kwanza ya kujijengea nidhamu ni kudhibiti fikra zako, kufikiri kama tayari umeshapata kile ambacho unakitaka. Huku siyo kujidanganya, bali ni kushinda mashaka yanayoweza kujengeka ndani yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha