Watu wengi wana ule mtazamo wa kizamani kwamba ili wewe ufanikiwe, lazima wengine washindwe. Ili wewe uwe tajiri, lazima wanaokuzunguka wawe masikini.
Huu ni mtazamo wa kizamani, ambao uliwazuia wengi wasifanikiwe, kwa sababu walihangaika na mambo ya wengine badala ya kuhangaika na mambo yao.
Mtazamo huo wa nyuma ulikuwa ni mtazamo wa uhaba, kwamba dunia ina uhaba wa rasilimali muhimu, hivyo ili upate wewe, lazima wengine wakose.
Mtazamo huu ulitengeneza ushindani wa mbwa kula mbwa (dog eat dog) na ushindani huu ulikuwa wa kubomoa badala ya kujenga.
Kwa sasa tuna maarifa bora kabisa, maarifa ambayo yamebadili kabisa mtazamo ambao tumekuwa nao kwa muda mrefu. Maarifa haya yanatuonesha kwamba kuna utele wa kila kitu, hivyo kila mtu anaweza kupata anachotaka bila ya mwingine kukosa.
Huna haja ya kuwanyang’anya wengine kile unachotaka wewe, bali unaweza kukipata kwa njia bora, huku wengine nao wakipata wanachotaka.
Mafanikio yako hayapaswi kuwa gharama kwa mtu yeyote yule, bali yanapaswa kuwa neema. Kufanikiwa kwako kunapaswa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na siyo kuwa hovyo.
Kama unategemea kufanikiwa kwa kuwaangusha wengine, upo kwenye njia ya kupotea, hata kama utafikia lengo hilo, hutaweza kulifurahia. Pia hutaweza kujiamini kwamba umepata mafanikio hayo kwa uwezo wako, bali utajua ni kwa kuwaharibia wengine, hivyo utakuwa na wasiwasi kwamba mwingine anaweza kukuharibia wewe pia.
Mafanikio ya kweli ni pale unapoyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi ya yalivyokuwa awali, na siyo kuyaharibu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,