Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali tunazopitia na zinazotuzuia tusifanikiwe. Changamoto siyo mwisho wa mipango yetu, bali ni njia ambayo tukiweza kuivuka itatuwezesha kwenda mbali zaidi.

Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza jinsi ya kujijengea nidhamu ya kufanya kile ambacho umepanga kufanya. Unaweza kuona ni rahisi, lakini hiki ndiyo kikwazo cha kwanza kwenye mafanikio ya wengi.

elimu fedha 2

Kabla hatujashauriana ni mambo gani ya kufanya, tupate maoni ya wasomaji wenzetu walioomba ushauri kwenye hili.

Nina mbinu za kufaulu mitihani lakini nashindwa kuzitumia. Nifanye nini ili niweze kuzitumia? – J. S. Mrisho

Mimi nashindwa kupanga ratiba ambayo itanifanya kukava topic vizuri kabla ya mtihani, ahsante – L. J. Maseke.

Ushauri huu umeombwa kwa upande wa masomo, lakini changamoto ya aina hii inawakumba wengi kwenye maeneo mbalimbali.

Mfano kuna watu wanaweza kuwa wanajiuliza maswali ya aina hii;

Nina mbinu zote za kufanikiwa kwenye maisha, lakini nashindwa kuzitumia kufanikiwa.

Nina mbinu zote za kufanikiwa kwenye biashara, lakini kila biashara ninayoanza inakufa.

Nina maarifa yote ya kupunguza uzito wa mwili, lakini kila nikipunguza uzito baada ya muda unarudi tena.

Kama unajua, kama mbinu zote unazo, lakini unashindwa kuzitumia au unazitumia lakini hupati majibu sahihi, basi tatizo ni nidhamu, hujaweza kujijengea nidhamu ya hali ya juu itakayokusukuma kufanya kile ambacho ni sahihi mara zote, bila ya kujali ni matokeo gani unayoyapata.

SOMA; Nguvu Hizi Tatu Zitakuwezesha Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha Yako.

Huwa nasema karibu kila mtu anajua ni nini anachotaka kwenye maisha yake, hilo halina tatizo.

Na katika wale wanaojua wanachotaka, wengi pia wanajua wanapaswa kufanya nini ili kupata wanachotaka.

Lakini inapofika kwenye kufanya kile wanachopaswa kufanya ili kupata kile wanachotaka kupata, ndipo wengi hukwama. Wengi hawana nidhamu ya kutosha kujisukuma wao wenyewe ili kuweza kupata matokeo wanayoyataka.

Ili kuweza kujijengea nidhamu hii, chukua hatua zifuatazo;

  1. Tengeneza utaratibu na ratiba yako ya siku.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanafanya ni kuianza siku kama dharura au ajali, kinachotokea ni kila kitu kinakuwa dharura. Unaimaliza siku ukiwa umechoka, lakini unapoangalia, hakuna matokeo makubwa ambayo umeyazalisha kwenye siku hiyo.

Unapaswa kutengeneza utaratibu wako wa siku (daily routine) ambao unakuwa ndiyo mwongozo mkuu unaouishi kila siku ya maisha yako. Hiyo inakuwa ndiyo ratiba kuu ya maisha yako, na unapanga kabisa ni muda gani unafanya nini.

Utaratibu wako wa siku unapaswa kueleza ni muda gani unaamka, ukiamka unafanya nini, na mambo mengine mpaka muda wa kulala. Yale mambo ambayo ni muhimu kwako yanapaswa kupata ratiba ya kudumu kwenye utaratibu wako wa siku.

Kwa mwanafunzi lazima kila siku uwe na muda uliotenga kwa ajili ya kujisomea, kwa anayetaka kupunguza uzito, lazima utaratibu wako wa siku uwe na muda wa kufanya mazoezi na ulaji sahihi.

Wakati utaratibu wa siku unaongoza kila siku yako, unapaswa pia kuwa na ratiba ya siku husika. Kila siku asubuhi, kabla siku yako haijaanza, panga mambo ambayo utakwenda kuyafanya kwenye siku yako hiyo (to do list). Mambo hayo yapange kwa kuyaorodhesha kabisa na hayo ndiyo utayafanya kwenye siku yako.

Utaratibu na ratiba yako ya siku vinapaswa kuwa karibu na wewe muda wote na uvielewe vizuri.

Usikubali kuendelea kuziendesha siku zako kama ajali au dharura, pangilia kila kitu na iendee siku yako kama ulivyopangilia.

  1. Fanya kile ulichopanga kufanya au usifanye chochote.

Najua unaweza kuwa unajiambia kwamba kupanga utaratibu na ratiba ya siku siyo shida kwako, huwa unapanga sana, lakini inapofika kwenye utekelezaji ndiyo unashindwa kutekeleza.

Na hapa nina habari njema kwako, ambazo zitakusukuma ufanye ulichopanga au zikufanye kuwa mjinga na upate uchoshi.

Tatizo letu ni moja, ni rahisi sana kwetu kuacha kufanya kile ambacho tumepanga kufanya, kwa sababu tunajiruhusu kufanya vitu vingine. Mfano ulipanga kusoma, lakini muda wa kusoma umefika na hujisikii kusoma, hivyo unachofanya ni kuchukua simu na kuingia kwenye mitandao ya kijamii mpaka pale muda wa kusoma unapoisha. Hilo halikuumizi kwa sababu muda unakuwa umepita bila ya wewe mwenyewe kujua.

Sasa, ili kuondokana na hali hiyo, fanya hivi; kwenye utaratibu na ratiba uliyojiwekea, fanya kile ulichopanga, na kama hujisikii kufanya basi usifanye chochote, kaa tu bila ya kufanya chochote.

Mfano umeweka kwenye ratiba yako kwamba kuanzia saa 12 mpaka saa 2 utasoma, unafika muda huo na hujisikii kusoma, hapo usikimbilie kushika simu au mengine. Muda huo unapofika, una machaguo mawili, kufanya kile ulichopanga au kutokufanya chochote. Yaani ukae tu mpaka muda huo utakapoisha.

Sasa kwa sababu sisi binadamu huwa hatupendi kukaa bila ya kufanya chochote, tutajisukuma kufanya tulichopanga kufanya. Fanya ulichopanga kufanya au usifanye chochote kabisa, usijipe njia rahisi ya kutoroka ulichopanga kufanya.

SOMA; Hatua Nne Za Kuizuia Simu Janja Yako Isikuzidi Wewe Ujanja.

  1. Punguza mambo ya kufanya, weka vipaumbele, ondoa usumbufu.

Tumejifunza kwamba unapaswa kuwa na utaratibu na ratiba ya siku, kwa kuorodhesha yale yote unayopanga kufanya kwenye siku yako. Kuna tahadhari muhimu unapaswa kuijua hapa, kwa sababu unapanga siku yako haimaanishi kila unachotaka kufanya utaweza kukifanya.

Unapaswa kuweka mambo machache muhimu kwenye utaratibu na ratiba yako ya siku. Orodha ya vitu unavyotaka kutekeleza viwe vichache na vilivyo muhimu zaidi.

Pia unapaswa kuhakikisha hakuna usumbufu unaoingilia kufanya kile ambacho umepanga kufanya, hivyo maandalizi yote yawe tayari kabla ya muda wa kufanya.

Simu, Tv, habari na hata mazungumzo ya watu wengine hakikisha hayaingilii ratiba yako ya siku.

Chochote ambacho siyo muhimu hakipaswi kupata muda wako.

Weka vipaumbele kwenye vile ambavyo vinakufikisha kwenye lengo laki, vingine nje ya hapo ni usumbufu kwako, usivipe nafasi.

  1. Weka nguvu kwenye mchakato na siyo matokeo.

Huwezi kusoma siku moja na ukafaulu mtihani, lakini ukisoma kila siku kwa mwaka mzima, utapata matokeo mazuri kwenye mtihani.

Huwezi kufanya mazoezi au dayati kwa siku moja na ukapunguza uzito, lakini ukifanya mazoezi na dayati kwa mwaka mzima, lazima uzito upungue.

Huwezi kuweka akiba kwa siku moja na ukaondoka kwenye madeni, lakini ukiweka akiba kila siku kwa mwaka mzima, utaunguza au kuondoka kabisa kwenye madeni.

Tunakwama kwa sababu tunaangalia matokeo na siyo mchakato. Tunaangalia nini tumepata wakati tumefanya kwa siku chache, na pale matokeo yanapokuwa tofauti na matarajio yetu, tunakata tamaa na kutoendelea kufanya.

Usiangalie matokeo, badala yake angalia mchakato. Usiangalie sana unapata nini, bali angalia zaidi unafanya nini.

Kama unachofanya ni sahihi, unafanya kama ulivyopanga, ni jambo la muda na uvumilivu tu, lazima upate kile unachotaka. Usikate tamaa pale unapoweka juhudi lakini hupati matokeo uliyotarajia, kama unafanya ulichopanga na unafanya kwa usahihi, jipe muda na endelea kufanya, utapata unachotaka.

SOMA; Kama Unataka Kufanikiwa 2020 Achana Na Malengo Na Kazana Na Kitu Hiki Kimoja.

  1. Kuwa na mtu wa kukusimamia na kukuwajibisha.

Kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, huwa hatupendi kujitesa wala kujiumiza, huwa tunapenda kutunza nguvu zetu badala ya kuzitumia. Hivyo unapopanga kufanya kitu, halafu unafika wakati wa kufanya kile ulichopanga, unapokutana na ugumu au changamoto, ni rahisi kwako kuacha kufanya.

Na hapo ndipo unapohitaji njia ya kukuzuia usiishie njiani, njia ya kukusukuma wewe kufanya kile ambacho umepanga kufanya.

Unaweza kutimiza hilo kwa kuwa na mtu wa kukusimamia na kukuwajibisha.

Kwa kukusimamia anahakikisha unafanya kile ambacho umepanga kufanya kwa namna ulivyopanga kufanya. Mtu huyo anapaswa kujali sana kuhusu wewe na hivyo kutokukuonea huruma pale unapotengeneza sababu za kutetea uvivu wako.

Pia mtu huyo anapaswa kuwa tayari kukuwajibisha pale unapokwenda tofauti na ulivyopanga. Hivyo unapaswa kupanga adhabu au hatua za mtu huyo kuchukua pale unapokwenda kinyume na mipango yako mwenyewe.

Unaweza kuweka jambo la kukudhalilisha pale unapokwenda kinyume na mipango yako, au ukaweka gharama utakayolipa unapofanya tofauti na ulivyopanga. Chagua adhabu ambayo ukiifikiria tu, unajisukuma kufanya ulichopanga. Pia changua mtu ambaye hatakuonea huruma kwa namna yoyote ile, kwa sababu anachotaka ni ukue na kupiga hatua.

Rafiki, ukifanyia kazi mambo haya tuliyojifunza hapa, utabadilika, utaanza kupanga nini unafanya na wakati huo unapofika unafanya kweli. Kumbuka haya hayataleta matokeo ya haraka, hivyo uvumilivu ni muhimu.

Nidhamu ni muhimu sana, huwezi kufanikiwa kama huna nidhamu, hivyo kazana kujijengea nidhamu na hiyo itakusaidia sana.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania