Rafiki yangu mpendwa,
Akiwa na miaka 11 na 12, Mike Tyson alikuwa mtoto mtukutu na aliyeshindikana.
Mazingira aliyokulia alikuwa kama mtoto wa mtaani na alishirikiana na makundi ya vijana wakubwa katika kupigana mitaani na hata kuiba.

Hilo lilipelekea afungwe jela ya watoto kwa lengo la kurekebishwa tabia. Huko nako aliendelea na ukorofi wake kitu kilichopelekea kila mtu kumkatia tamaa na kuona maisha yake ataishia kuwa mhalifu tu.

Akiwa na miaka 13, Mike Tyson alikutana na mtu aliyeyabadili kabisa maisha yake na kumwezesha kuwa bondia mkubwa duniani.  Mtu huyo alikuwa ni Constantine D’Amato, ambaye akikuwa kocha wa mabondia mbalimbali waliofanya vizuri.

D’Amato alipokutana na Tyson kwa mara ya kwanza na kumuona akiwa anapigana, alisema wazi kwamba huyu atakuja kuwa bingwa wa dunia. Alisema ndani yake ameona uwezo mkubwa na pia ana shauku ya kufanya makubwa kwenye maisha yake.

Lakini aliona matatizo makubwa matatu ya Tyson ambayo yalikuwa kikwazo kwake.

Tatizo la kwanza ilikua mtazamo, alikuwa na mtazamo mbaya kutokana na aliyopitia, hivyo D’Amato alifanya kazi kubwa ya kubadili kabisa mtazamo wake.

Tatizo la pili alikuwa na tabia mbovu ambazo ndiyo zilimpeleka kwenye uhalifu, hapo D’Amato aliweka nguvu kuzivunja kabisa tabia hizo.

Tatizo la tatu hakuwa na ujuzi sahihi, D’Amato alimfundisha mbinu ya kupigana inayoitwa peek-a-boo ambayo ilimsaidia sana.

Haikuwa rahisi kufanyia kazi hayo matatu, ilimchukua Tyson miaka 6 ya kuweka juhudi kubwa na kusukumwa sana na kocha wake D’Amato mpaka kuweza kufikia ubingwa wa dunia.

Na kama D’Amato alivyotabiri, Tyson aliweza kuwa bingwa wa dunia, kwa kuweka rekodi ya kushika taji hilo katika umri mdogo. D’Amato alifariki mwaka mmoja kabla ya Tyson kupata ubingwa huo.

Katika mahojiano mengi na hata kwenye kitabu chake kinachoitwa IRON AMBITION, Tyson anaeleza wazi kwamba ni D’Amato aliyeyabadili maisha yake na kumjenga kwa namna alivyoweza kukua.

Na hata alipoanguka kutoka kwenye ubingwa, Tyson anakiri kama D’Amato angekuwa hai hilo lisingetokea. Anasema hakuna mtu angeweza kumshinda hapa duniani kama D’Amato angekuwa hai.

Wachezaji wote wenye mafanikio makubwa sana huwa kila mtu anajua majina yao, maana ndiyo wanaoshinda mataji mbalimbali.
Lakini nyuma ya kila mchezaji mwenye mafanikio makubwa, kuna mtu ameweka juhudi kubwa kumfanya vile alivyo.
Mtu huyo ni kocha wake, ambaye anakuwa na imani kubwa kwake.

Hakuna mchezaji mwenye mafanikio asiye na kocha. Kocha ana nafasi kubwa kwa mafanikio ya mchezaji kwa sababu anayaona madhaifu aliyonayo mchezaji na kumsaidia ili yasiwe kikwazo kwake.

Pia kocha anakuwa na imani kubwa kwa mchezaji, kitu kinachomfanya mchezaji naye ajiamini pia.

Na zaidi, kocha anamsukuma mchezaji kuondoka kwenye uvivu, uzembe na mazoea ili aweke juhudi ba kufanya vizuri.

Inapokuja kwenye michezo watu wanajua kabisa umuhimu wa kocha, lakini inapokuja kwenye maisha, kazi, biashara na mafanikio kwa ujumla, watu wanaona wanaweza kufanikiwa peke yao tu.

Huko ni kujidanganya, ni vigumu mno kufanikiwa ukiwa peke yako.
Hata ukiangalia wale waliofanya makubwa kwenye maisha, walikuwa na washirika ambao ni bora kabisa au walikua na makocha au mamenta waliowasukuma kufanya makubwa.

Kwa asili sisi binadamu ni wavivu, wazembe, tunaopenda kufanya kwa mazoea na kuridhika haraka.
Tunapenda raha za muda mfupi kuliko kuteseka ili kuja kupata furaha ya muda mrefu.

Hii ni asili yetu kabisa, ni vigumu sana kuweza kupambana nayo peke yako na kuishinda.
Unahitaji mtu mwingine wa kushirikiana naye ili uweze kuvuka asili hiyo.

Mtu ambaye utamuahidi nini unafanya na kufuatilia kuhakikisha kweli unafanya.
Mtu ambaye anapitia kila unachofanya na kukuonyesha maeneo ya kuboresha zaidi.
Mtu ambaye atakusukuma kuondoka kwenye mazoea na kutokuridhika haraka.

Rafiki, unamhitaji sana kocha kwenye maisha yako, kuliko unavyodhani.
Watu wengi wamekuwa wabishi kwenye hili kwa sababu ya ujuaji mwingi, kuona tayari wanajua kila kitu.
Wengine kwa sababu ya kiburi na ufahari, kuona kama ni udhaifu kusimamiwa na mtu mwingine.

Rafiki, usiingie kwenye kundi hilo, kwani ni wajuaji sana ambao huwa hawafanikiwi kwenye maisha yao. Ni wenye kiburi ambao hurudia makosa yale yale mpaka kuishia kwenye anguko.

Kama upo makini na maisha yako na kama unataka kufanya kitu cha tofauti hapa duniani, huwezi kwenda peke yako, unahitaji kuwa na kocha.

Mambo ya kufanya ukishakuwa na kocha.

Kuwa na kocha peke yake haitoshi wewe kufanya makubwa. Ni pale unapomtumia kocha kwa usahihi ndiyo unaweza kufanya makubwa.
Hapa ni yale muhimu unayopaswa kufanya ukishakuwa na kocha.

1. Unapaswa kumwamini kocha wako na yeye pia akuamini. Bila ya kuaminiana ushirikiano hauwezi kuwa mzuri.

2. Unapaswa kuwa muwazi kwa kocha wako, ajue wapi unataka kufika na changamoto zipi unakabiliana nazo. Usimfiche chochote kocha wako kwa sababu kila unachopitia kinaweza kuwa na athari kwenye matokeo unayotaka kufikia.

3. Unapaswa kumsikiliza kocha wako, kujifunza yale anayokushirikisha na kuchukua hatua ili kuleta matokeo ya tofauti.

4. Unapaswa kumuuliza maswali kocha wako ili ujue kwa kina kile unachofanya na namna ya kufika unakotaka kufika.

5. Unapaswa kuijua na kuiishi falsafa ya kocha wako, ili hata siku akiwa hayupo tena, ubaki kuwa imara na siyo kuanguka.

Kwa kuzingatia hayo matano, utaweza kunufaika sana na kocha unayekuwa naye. Hutabaki pale ulipo kama utakuwa na kocha na kuzingatia hayo muhimu.

Swali muhimu kwako.
Rafiki yangu mpendwa, hapa nina swali muhimu sana kwako ambalo naomba unijibu kwenye maoni hapo chini.
Je nani ni kocha wako?
Na je unamtumiaje kocha wako kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako?
Nasubiri majibu yako ili tuweze kujadiliana na uondoke na hatua bora za kuchukua na maisha yako yanufaike sana.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz

Ndani yako unayo nguvu ya kuweza kufanya makubwa zaidi ya ulivyozoea. Pata na usome kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA ujifunze jinsi ya kuifikia na kuitumia nguvu iliyo ndani yako. Kukipata wasiliana na 0752 977 170