Kumekuwa na malalamiko mengi ya watu kuhusu mafanikio.

Kuna wale ambao wanajitoa maisha yao yote, wanaachana na kila kitu kwa ajili ya kufikia lengo fulani, wakiamini kwamba wakishafikia lengo hilo, watakuwa na furaha maisha yao yote na hawatahitaji kujisumbua tena.

Halafu kuna wale ambao wamezaliwa kwenye mafanikio, kitu ambacho kinawafanya wasijisukume kwa ajili ya chochote na hilo linawafanya kuwa wazembe na kushindwa kufanya makubwa kwenye maisha yao.

Malalamiko yote haya kuhusu mafanikio yanakuja kwa sababu watu wana mtazamo usio sahihi kuhusu mafanikio.

Wengi wanafikiri kwamba kufanikiwa ni kutokuwa na kitu kinachokusumbua, kutokuwa na changamoto kabisa, kila kitu kinaenda kama unavyotaka.

Huo siyo mtazamo sahihi, maisha yetu yanapewa maana na magumu au changamoto ambazo tunapitia. Kila tunapokutana na ugumu na tukapambana kuuvuka, hapo ndipo maisha yetu yanapata maana na tunayafurahia.

Lakini pale ambapo hatukutani na ugumu wowote, kila kitu kinaenda kama tunavyotaka, tunapata uchoshi kwenye maisha, tunaona maisha hayana maana na mafanikio hayana furaha. Tunaweza kwenda mbali zaidi hata kutengeneza matatizo ili tu kuyaweka maisha yetu kwenye hali ya kutatua kitu. Hivi ndivyo watu wanavyoingia kwenye ulevi na mambo mengine.

Kama unataka kuwa na maisha bora, kama unataka kuwa na mafanikio utakayoyafurahia, hakikisha kila wakati kuna changamoto unayoifanyia kazi kwenye maisha yako. Hakikisha kuna kitu kikubwa unachopambana kukifanyia kazi au kukifikia, kitu kinachokunyima usingizi.

Na ukikifikia hicho, weka mpango wa kingine. Kwa kifupi, kila wakati kuwa na lengo kubwa unalofanyia kazi, ukilifikia, weka lengo jingine kubwa zaidi ya hilo la awali.

Maisha yasiyokuwa na kitu kikubwa kinachokusukuma ni maisha yanayochosha, usijaribu kuwa na maisha ya aina hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha