Sababu kubwa inayopelekea watu kuahirisha mambo ni kwa sababu hawana uhakika wa matokeo wanayokwenda kupata.

Pata picha unahitaji kuwatembelea wateja kuwaeleza kuhusu bidhaa au huduma yako, lakini huna uhakika kama watakubali na kununua au la. Unapoongea na wateja wachache na wakakuambia hapana, ni rahisi kuahirisha, kujiambia utaendelea siku nyingine na kutafuta kingine cha kufanya ambacho una uhakika na matokeo yake.

Upande mwingine pata picha unakwenda kumtembelea mteja mmoja ambaye amekuhakikishia atanunua na unajua ni mwaminifu, hapa hutakuwa tayari kuahirisha chochote, utafanya kila namna mpaka umfikie mteja huyo, kwa sababu una uhakika wa matokeo.

Sasa unaweza kulitumia hili kwenye maisha yako ya kawaida, kwa chochote unachokifanya, jitengenezee uhakika wa matokeo utakaokusukuma kuchukua hatua.

Mwandishi na mhamasishaji mashuhuri Tonny Robins anasema alianza huduma yake kwa kuuza mafunzo ya aliyekuwa mhamasishaji mashuhuri Jim Rhon. Alikuwa akipita nyumba kwa nyumba kutafuta wateja. Alichofunza ni kwamba, ili auze kwa watu watatu, bali anahitaji kutembelea wateja kumi. Hivyo alikuwa anapata ndiyo 3 na hapana kumi. Alipiga faida anayopata kwenye mauzo na kuigawa kwenye hapana hizo. Kisha alipokuwa anakutana na mteja na kumwelezea kuhusu anachouza, pale mteja alipoanza kuonesha dalili za kukataa, Tonny alimwambia, wewe sema hapana na nitapata dola 10 (faida ya kila hapana). Hili lilimsukuma sana, hakuona tena hapana kama kitu kibaya, bali kama njia ya kumfikisha kwenye lengo.

Tujifunze kupitia hilo, tafuta matokeo yoyote unayoweza kuyapata na yageuze kuwa faida kwako, kisha tumia matokeo hayo kujisukuma zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha