Farasi wa kuchonga anaweza kuwafurahisha watu kwa jinsi alivyochongwa vizuri, lakini kama unataka kwenda mahali na farasi, basi unahitaji farasi aliye hai, haijalishi anafurahisha watu au la.
Kwenye maisha, kuna vitu vinatufurahisha, lakini haviwezi kutupeleka popote, tunafurahia kuviona, tunafurahia kuvifanya, tunafurahia kuvifuatilia na kuvizungumzia, lakini haviwezi kutupeleka popote.
Kuanzia sasa anza kufuatilia vitu unavyofanya na jiulize je huyu ni farasi aliye hai au wa kuchongwa? Kama kitu hakikufikishi kule unakotaka kwenda, hapo unahangaika na farasi wa kuchongwa, na usije ukamlalamikia yeyote kwa nini hufiki unakotaka kufika, kwa sababu wewe mwenyewe umechagua kuhangaika na farasi wa kuchonga.
Tukiendelea na mfano huu wa farasi, utakubaliana nami kwamba huhitaji nguvu nyingi kukaa na farasi wa kuchongwa, yaani huhitaji nguvu yoyote, yuko hapo, ni wewe kumfurahia tu. Lakini farasi aliye hai, atakutoa jasho, utahitaji nguvu kuweza kumweka sehemu moja, utahitaji kumlisha na kujali mambo mengine yanayomhusu.
Hivyo kama kuna kitu unachofanya ambacho hakihitaji juhudi zako, jua unahangaika na farasi wa kuchongwa na hivyo hana nguvu ya kukupeleka popote.
Usihangaike na farasi wa kuchongwa, hangaika na farasi walio hai, maana unachohitaji kwenye maisha siyo kufurahia vitu, bali kufika kule unakotaka kufika.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,