Ni vita ya kujitambua, kila wakati unafanya makosa fulani yanayotokana na kutokujitambua vizuri.

Hivyo ukijiambia kwamba umeshajitambua, maana yake ni umekubali kushindwa vita hiyo.

Unaweza kuona unafanya kitu sahihi, lakini kikawa siyo sahihi.

Hii ni kwa sababu sisi binadamu tuna madhaifu makubwa mawili;

Udhaifu wa kwanza ni ufahari au majivuno. Huwa tunapenda kufanya mambo ambayo yanatupa sisi ufahari au kuwa na majivuno. Hivyo tunaweza kufikiri tunachofanya ni sahihi, kumbe tunasukumwa tu na kutaka ufahari.

Udhaifu wa pili ni upofu, kuna vitu viko wazi kabisa kwa wengine, lakini sisi hatuvioni. Kila mtu kuna eneo ambalo ana upofu. Unaweza kufanya maamuzi ukijua ni sahihi, kumbe upofu wako umekuzuia usione uhalisia.

Ili kuvuka madhaifu haya, na ili kutokushindwa vita hii ya kujitambua, lazima kila wakati na kwa kila jambo ujifanyie tathmini. Kwa kila unachofanya anza kwa msukumo unaokufanya ukifanye, ni nini hasa kinachokusukuma? Acha yale unayowadanganya wengine kwa nje, jipe jibu sahihi kutoka ndani yako. Unaweza kuwa unatoa msaada, kwa nje unawaonesha watu kwamba unajali, lakini kwa ndani unataka uonekane. Jua msukumo uliopo ndani yako na hapo utaweza kujua kipi sahihi kufanya.

Kitu cha pili cha kufanyia tathmini ni makosa unayofanya. Kila kosa unalofanya likubali, halafu jiulize umefikaje kwenye kosa hilo. Kipi ambacho hukukiona hapo awali, msukumo gani uliokuwa nao na hata matarajio uliyojiwekea. Ukifanya tathmini kwenye kila kosa unalofanya, utaona wazi makosa ambayo umekuwa unayafanya na hivyo kujiepusha usiyarudie tena.

Hakuna mtu aliyekamilika, hakuna aliyejitambua kwa asilimia 100, maisha yetu ni mchakato, kujitambua ni swala endelevu. Hivyo kila siku kazana kuwa bora zaidi ya siku iliyopita na utaweza kupunguza matatizo na changamoto mbalimbali unazokutana nazo kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha