Kuna kujitambua kwa kawaida (self-awareness), hapa ni pale unapojua madhaifu yako, uimara wako na kuweza kujiangalia wewe mwenyewe kama unavyoweza kumwangalia mtu mwingine. Unapofikia kujitambua huku, ni rahisi kuona makosa unayoyafanya na kuwa bora zaidi.
Halafu kuna kujitambua kwa hali ya juu (self-actualization), hapa ni pale unapoenda juu zaidi ya kujua uimara na madhaifu yako, unapovuka makosa yako na kufika viwango vya juu kabisa vya maisha yako.
Kujitambua kwa hali ya juu kuna sifa kuu mbili.
Sifa ya kwanza ni kuwa na maadili ambayo unayaishi na kuyasimamia kila siku. Katika kila hali, unayasimamia maadili hayo na hukubali kuyavunja kwa namna yoyote ile. Maadili haya unakuwa umeyachagua au kuyapokea na kuyakubali wewe mwenyewe na siyo kulazimishwa na mtu yeyote yule. Kuwa na maadili unayoyasimamia, kunakuepusha usifanye makosa mbalimbali.
Sifa ya pili ni kulijua kusudi la maisha yako na kuliishi kila siku. Hapa unakuwa umejua kwa nini uko hapa duniani, na kila siku unatekeleza kile kilichokuleta duniani. Kwa kuliishi kusudi lako, kila siku unaridhika na maisha yako, kwa sababu kila unachofanya kinakuwa na maana kubwa kwako na mchango bora kwa wengine. Unapofanya kile ambacho ni kusudi lako, haiwi mzigo kwako na wala huchukulii kama kazi, bali unachukulia kama kutimiza wajibu wa wewe kuwa hai.
Kuweza kuishi sifa hizi mbili, lazima uwe na ujasiri mkubwa, uwe tayari kuonekana wa tofauti na wa ajabu, uwe tayari kusimama peke yako hata pale kila mtu anapokuwa anapingana na wewe. Lakini uzuri ni kwamba, mwisho wa siku watu watakuelewa na watakuwa upande wako.
Ni wachache sana ambao wanafikia utambuzi huu wa juu, siyo kwa sababu ni mgumu kufikia, bali kwa sababu unahitaji nidhamu na uthubutu, vitu ambavyo wengi hawana.
Chagua leo kufikia utambuzi wa juu, chagua maadili utakayoyaishi na jua kusudi la maisha yako na liishi kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana kocha kwa makala hii nzuri, endelea kutufungua akili zetu.
LikeLike