‘Say thank you every day. Say I am sorry every day. Say I love you every day.’

Ni siku nyingine nzuri, siku mpya na ya kipekee kwako kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Maisha yetu hayawezi kukamilika kama tupo peke yetu,
Tunawahitaji watu wengine kwenye safari hii ya mafanikio.
Hivyo upendo ndiyo nguzo muhimu inayotuwezesha kwenda pamoja na wale ambao tunawahitaji.

Upendo ni kitu ambacho kinapaswa kuanzia ndani ya mtu mwenyewe na kuwa tayari kukitoa kwa wengine.
Upendo halisi hauwi na sababu, bali upendo wenyewe ni sababu.
Na upendo ni kitu cha kuishi kila siku, na siyo kwa siku fulani fulani pekee.

Kidunia leo ni siku ya wapendanao, lakini kwetu wanamafanikio, kila siku ni siku ya wapendanao.
Unafikiri ni kitu gani kitakusukuma kufanya makubwa kama siyo upendo?
Kitu gani kikuamshe asububi na mapema, kikucheleweshe kulala, kikunyime starehe ambazo wengine wanazifurahia kama siyo upendo?

Ni upendo kwetu sisi wenyewe, upendo kwa wengine na upendo kwenye kile tunachofanya ndiyo unatusukuma kufanya makubwa zaidi, unafanya maumivu yetu yawe na maana, kushindwa kwetu kuwa sehemu ya kujifunza na mateso yetu kuwa ushindi.
Kwa kuwa upendo ni kitu tunachokiishi kila siku, kuna maneno matatu muhimu sana ya kuwaambia wale uwapendao.
Maneno hayo ni NAKUPENDA, ASANTE na SAMAHANI.
Maneno rahisi lakini yamebeba nguvu kubwa sana ndani yake.

Waambie wale ambao unawapenda kwamba UNAWAPENDA, hili ni zoezi la kila siku na siyo kusubiri siku fulani fulani.
Waambie watu ASANTE, kwa chochote wanachofanya au kusema na kikawa na mchango au umuhimu kwako. Hili ni kila siku na kila wakati.
Na pale unapowakwaza wengine au kukosea, sema SAMAHANI, inawafanya waone unajali na hukufanya kwa kukusudia.

Maneno hayo matatu hayahitaji elimu kubwa uweze kuyasema,
Hayakugharimu chochote kuyasema,
Lakini matokeo yake ni makubwa na bora sana.
Angalizo; lazima uyaseme ukimaanisha kweli na siyo kwa kuigiza ili kupata unachotaka. Sisi binadamu tupo vizuri sana kwenye kujua ukweli na maigizo.

Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kusema NAKUPENDA, ASANTE na SAMAHANI, maneno matatu ya kutumia kila siku.

Kocha akupendaye,
Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania