Tunaathiriwa na kushawishiwa zaidi na mazingira kuliko tunavyoweza kuamini na kukubali.

Huwa tunafikiri maamuzi mengi tunayofanya ni kwa kufikiri sisi wenyewe, lakini siyo kweli, kwa sehemu kubwa tunafuata ushawishi wa mazingira na wale wanaotuzunguka.

Tafiti zinaonesha kwamba kadiri bidhaa au huduma inavyokuwa karibu na sisi au tunavyoiona mara kwa mara ndivyo tunavyokuwa tayari kuitumia.

Ukifika eneo ambalo ni geni na hujui ufanye nini, utaangalia kile wengine wanafanya na utaanzia hapo.

Na kingine cha kushangaza na kustaajabisha zaidi, kama wengine wanafanya makosa na wewe uko sahihi, ni rahisi sana na wewe kufanya makosa. Kama watu wawili na zaidi wanafanya kitu ambacho siyo sahihi kwa kujiamini, na wewe unafanya kilicho sahihi, ni rahisi kuacha kulicho sahihi na kufanya kisicho sahihi.

Mazingira yetu, yana ushawishi na athari kubwa sana kwetu, hivyo kama tunataka kufanya maamuzi sahihi na bora kwetu, tunapaswa kuanza na kudhibiti mazingira yetu na wale wanaotuzunguka.

Jua kila ushawishi uliopo kwenye mazingira yako kabla hujafanya maamuzi yoyote. Ukiangalia baada ya kufanya maamuzi unakuwa umeshachelewa, na utajidanganya kwamba umefanya maamuzi sahihi.

Chukua mfano huu rahisi, umetoka nyumbani, hukuwa na mpango wa kununua nguo, ukiwa unapita nje ya maduka ya nguo, unaona tangazo, punguzo la nusu bei, ukaingia na kununua. Hapo ni mazingira yamekushawishi na kukuathiri, kuliona tangazo la nusu bei kumechochea wewe kufikia maamuzi hayo. Kama ungepita njia nyingine au kama usingeona tangazo hilo, usingefanya maamuzi hayo, maana hukutoka na mpango huo nyumbani.

Huu ni mfano mmoja, lakini vitu vingi unavyofanya kwenye maisha yako, unashawishiwa na kuathiriwa na mazingira na wale wanaokuzunguka. Anza kudhibiti vitu hivi na utaweza kufanya maamuzi bora kabisa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha