Kwa jambo lolote baya unalokutana nalo au linalotokea kwenye maisha yako, kumbuka kwamba mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi ya yalivyo sasa. Kwa kujikumbusha hili, hutalaumu, badala yake utashukuru na hilo kitakuwezesha kutoka ulipokwama sasa.
Unaumwa? Hebu fikiria wale ambao wapo hoi kuliko wewe, au ambao wamefariki dunia. Unaweza kuona kuumwa ni jambo baya na kubwa kwako, lakini ukiangalia nini kibaya zaidi kinaweza kutokea, utashukuru kwa hali uliyonayo sasa.
Umefukuzwa au kupoteza kazi? Ndiyo ni jambo baya kutokana na kuitegemea kazi hiyo moja kwa moja. Lakini hebu fikiria kama ungepoteza mikono yako miwili, au miguu yako, je mambo yangekuwaje? Makubwa na magumu zaidi. Hivyo kupoteza kazi huku una mwili na akili yako vikiwa sawa, ni jambo la kushukuru, kwa sababu unaweza kupata kazi sehemu nyingine na maisha yakaendelea.
Umepata hasara kwenye biashara, ni jambo kubwa na linaloumiza, lakini fikiria wale ambao biashara zao zinakufa kabisa, hapo utaona kupata hasara huku biashara yako ikiwa hai ni jambo la kushukuru, maana unajifunza mambo ya kuepuka ili usirudie tena kupata hasara.
Kila jambo unalokutana nalo, haijalishi ni baya kiasi gani, lingeweza kuwa baya zaidi ya hapo. Hivyo usiwe mtu wa kukimbilia kulalamika na kulaumu, bali angalia ni jinsi gani jambo hilo lingeweza kuwa baya zaidi, kisha shukuru.
Unaposhukuru unaiambia dunia kwamba umejifunza kitu na upo tayari kuwa bora zaidi. Unaposhukuru maana yake umekubali mchango wako kwenye jambo ulilokutana nalo na upo tayari kurekebisha. Lakini unapolaumu au kulalamika, unaeleza wazi kwamba huhusiki, umeonewa tu, na kwa hakika ni kwamba dunia hua haimuonei mtu yeyote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,