Kuna wakati unahitaji kukaa kimya hata kama upo sahihi na kuacha upande usio sahihi kuendelea na mambo yao.
Hii siyo kukubaliana na upande huo, bali kuepuka vita ambayo ushindi wake hautakuongezea chochote.
Kuna wakati unahitaji kuwaacha wale ambao hawapo sahihi wajifunze kwa makosa yao wenyewe, kwa kuumia na siyo wewe kuwahubiria kwa nini hawako sahihi.
Kuwa sahihi kila wakati na kutaka kuonekana hivyo ni njia ya uhakika ya kuharibu mahusiano yako na wengine.
Hii haimaanishi kwamba uwe mnafiki, ili tu kuwafurahisha wengine, bali kuepuka kuwa na vita hata kwenye mambo madogo madogo.
Hii haimaanishi ukiuke maadili na misingi yako ili kuwafurahisha wengine, bali kuwaacha wengine wachague maadili na misingi yao, kwa namna wanaona ni sahihi kwao.
Kumbuka wewe siyo kiranja wa dunia, na ukifa leo dunia haitasimama, hivyo jipe muda wa kuhangaika na yale muhimu na achana na mambo madogo madogo yatakayokunyima amani na utulivu.
Huu ni ujumbe muhimu sana kwetu sote ambao tuna misingi tunayoiishi, ambayo hatupo tayari kuivunja. Lakini huwa tunajisahau na kutaka wengine nao waishi misingi hiyo, hapo ndipo changamoto zinapoanzia.
Simamia misingi yako utakavyo, lakini usitake kila mtu afuate misingi hiyo, usilazimishe kila mtu afikiri kama wewe au kuona kama wewe. Wape watu ruhusa ya kuwa wao, hata kama wanakosea, muhimu ni usiruhusu mambo madogo madogo kukusumbua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,