Mapiramidi ya Misri ni moja ya maajabu makubwa ya dunia, kwa sababu ni kitu kikubwa kabisa kuwahi kujengwa na binadamu, tena katika wakati ambao hakukuwa na mashine za kurahisisha kazi kama zilizopo sasa.
Mapiramidi haya hayakujengwa kwa siku moja, yalijengwa kwa miaka.
Lakini ujenzi wake ulikuwa unafanyika kila siku, kwa kujirudia bila kuacha.
Hapa kuna somo kubwa sana kuhusu mafanikio, ni rahisi kusema mafanikio hayajengwi siku moja, lakini tunasahau kwamba mafanikio yanajengwa kila siku.
Kila unachofanya kwenye siku yako, kinajenga au kubomoa mafanikio yako.
Mafanikio hayana kilele, kwamba ukifika hatua fulani umemaliza kabisa. Kila siku ni siku ya kuendelea na mapambano.
Siku utakayojiambia kwamba umefika kwenye kilele ndiyo siku ambayo utaanza kuporomoka.
Kadhalika kwenye kujijengea tabia yoyote, siyo zoezi la siku moja na hakuna siku utafika na kusema umeshabobea kwenye tabia hiyo. Kwa sababu siku utakayoacha kufanya tabia hiyo, ni siku ambayo unaacha kuwa mtu anayefanya tabia hiyo.
Fanya kila siku, ndiyo kanuni sahihi ya kufanikiwa kwenye maisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,