Sisi binadamu huwa tunapenda kutumia nguvu kwenye kila jambo, kitu ambacho hakitupi matokeo mazuri mara zote.

Lakini kupitia falsafa mbalimbali, tunajifunza hekima ambayo tukiweza kuitumia, tunaweza kufanya makubwa bila ya kutumia nguvu sana.

Moja ya falsafa inayoweza kutupa nguvu ya aina hii, ni falsafa ya Taoism, falsafa ya kale ya china ambayo inaelezea Njia kuu ya maisha ambayo inaitwa Tao.

Njia hii ndiyo inayoiongoza dunia, ambapo mtu akiielewa njia hiyo, ataweza kufanya makubwa bila ya kutumia nguvu.

Mwanafalsafa Lao Tzu, aliandika kitabu kinachoitwa TAO TE CHING, kitabu kifupi sana lakini ambacho kinaielezea falsafa hii kwa kina. Kitabu hicho kina misingi muhimu sana ambayo ukiielewa na kuiweka kwenye maisha yako, utakuwa na maisha bora na yenye utulivu mkubwa bila ya kutumia nguvu nyingi.

tao te ching.jpg

Kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kuna tafsiri kamili ya kitabu hiki cha TAO TE CHING, unaweza kuingia kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania na ukapata falsafa hii bora kabisa kwa maisha yako.

Hapa nakwenda kukushirikisha sentensi fupi fupi kutoka kwenye kitabu hicho, ili uweze kuona jinsi kinavyoweza kuwa na manufaa kwako na utenge muda wa kusoma tafsiri ya Kiswahili ya kitabu hicho.

Karibu ujifunze misingi hii ya falsafa ya Tao ili uweze kuwa na maisha bora.

 1. Mkuu anatenda bila ya kufanya chochote,

Anafundisha bila ya kusema chochote.

Vitu vinaibuka na anaviruhusu vije, vinaondoka na anaviacha viende.

Anakila kitu lakini hamiliki chochote, anachukua hatua lakini hategemei chochote.

Akishafanya kazi, anaisahau, na ndiyo maana kazi yake inadumu milele.

 1. Kwenye makazi ishi karibu na ardhi.

Kwenye kufikiri rahisisha.

Kwenye ugomvi simama upande wa haki.

Kwenye kuongoza usidhibiti.

Kwenye kazi fanya unachopenda.

Kwenye maisha ya familia hakikisha unakuwepo.

Unapokuwa umeridhika na kuwa wewe, unapokuwa hujilinganishi wala kushindana na wengine, kila mtu atakuheshimu.

 1. Tunatengeneza mfinyanzi kuwa chungu, lakini ni utupu ndani yake unaohifadhi kile tunachoweka.

Tunatumia mbao kutengeneza nyumba, lakini ni nafasi ya ndani ndiyo tunayoishi.

Tunafanya kazi na vitu, lakini tunachotumia ni kisicho kitu (utupu).

 1. Kiongozi bora ni yule anayetawala bila ya watu kujua kama yupo.

Anayefuatia ni yule anayependwa.

Anayefuatia ni yule anayeogopwa,

Na kiongozi mbovu kabisa ni yule anayedharauliwa.

Kama huwaamini watu, unawafanya wasiwe waaminifu.

Mkuu haongei, anatenda.

Anapofanya kazi yake watu wanasema ni ajabu, tumeifanya wenyewe.

 1. Kama unataka kuwa mkamilifu, jiruhusu kutokuwa mkamilifu.

Kama unataka kuwa mnyoofu, jiruhusu kukosea.

Kama unataka kujaa, jiruhusu kuwa tupu.

Kama unataka kuzaliwa upya, jiruhusu kufa.

Kama unataka kupewa kila kitu, toa kila kitu.

 1. Kuna wakati wa kuwa mbele,

Wakati wa kuwa nyuma,

Wakati wa kuwa kwenye mwendo,

Wakati wa kupumzika,

Wakati wa kuwa na nguvu,

Wakati wa kuchoka,

Wakati wa kuwa salama,

Wakati wa kuwa hatarini.

Mkuu anaviona vitu kama vilivyo, bila ya kujaribu kuvidhibiti.

Anaviacha vifuate mkondo wake, na yeye anakaa katikati ya duara.

 1. Kuwajua wengine ni akili, kujijua mwenyewe ni hekima ya kweli.

Kuwatawala wengine ni nguvu, kujitawala mwenyewe ni nguvu ya kweli.

Ukitambua kwamba unavyo vya kutosha, wewe ni tajiri kweli.

Ukikaa katikati na kupokea kifo kwa moyo wako wote, utadumu milele.

 1. Mkuu hahangaiki kupata madaraka, hivyo anakuwa mwenye madaraka ya kweli.

Mtu wa kawaida anakazana kupata madaraka, na hapati madaraka ya kumtosha.

Mkuu hafanyi chochote, lakini hakuna anachoachwa hakijafanywa.

Mtu wa kawaida anafanya vitu mara zote, lakini kuna vingi anaacha havijafanywa.

 1. Umaarufu au uadilifu; kipi muhimu zaidi?

Pesa au furaha; kipi chenye thamani zaidi?

Mafanikio au kushindwa; kipi kinaharibu zaidi?

Kama mafanikio yako unajilinganisha na wengine, kamwe hutafanikiwa.

Kama furaha yako inategemea fedha, kamwe hutakuwa na furaha.

Ridhika na kile ulichonacho, furahia jinsi vitu vilivyo.

Unapotambua kwamba hakuna unachokosa, ulimwengu wote unakuwa wako.

 1. Njia kuu ni rahisi, lakini watu hupendelea njia za pembeni.

Tambua wakati mambo yanaenda nje ya usawa, na ukae katikati ya Tao.

Pale wachuuzi wanapotajirika wakati wakulima wanapoteza ardhi,

Pale viongozi wa serikali wanapotumia fedha kununua silaha badala ya tiba,

Pale matajiri wanapoishi kwa anasa huku masikini hawana pa kugeukia,

Huu wote ni wizi na machafuko,

Haiendani na Tao.

 1. Mito yote inaishia baharini, kwa sababu bahari iko chini kuliko mito.

Unyenyekevu ndiyo unaipa bahari nguvu.

Kama unataka kuwatawala watu, jiweke chini yao.

Kama unataka kuwaongoza watu, jifunze jinsi ya kuwafuata.

Mkuu yupo juu ya watu, lakini hakuna anayejiona amekandamizwa,

Anakuwa mbele ya watu, lakini hakuna anayeona amelaghaiwa.

Dunia nzima inashukuru kwa ajili yake.

Kwa kuwa hashindani na yeyote, hakuna anayeweza kumshinda.

 1. Kodi inapokuwa kubwa, watu wanasumbuka kwa njaa.

Serikali inapoanza kuingilia maisha ya raia wake, wanapoteza utu na imani yao.

Tenda kwa faida ya wengine, waamini na waache wafanye yao.

Hii ni sehemu ndogo ya hekima nyingi zinazopatikana kwenye kitabu cha TAO TE CHING. Unaweza kupata hekima zote kwa kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua hapa kujiunga; https://www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania