Watu wengi huwa wanajinasa kwenye mtego wa utumwa bila ya wao wenyewe kujua.

Unajiambia kwamba unataka kuwa huru, hivyo unajituma sana kwa kila namna kuhakikisha unafikia uhuru huo.

Kwa bahati mbaya, baadhi ya vitu unavyofanya ili kupata uhuru, vinakuwa ndiyo kuzika uhuru wako.

Mfano unataka kujenga biashara kubwa ili uwe huru kifedha, lakini katika kufanya hivyo, unatumia njia fulani zisizo sahihi.

Unaweza kukuza kweli biashara yako, lakini baada ya hapo, zile njia zisizo sahihi ulizotumia zitakuwa zinakunyima uhuru. Kuna watu watazijua na watakuwa wanazitumia kukulazimisha wewe ufanye wanachotaka wao, kwa sababu ukikataa, wataweka wazi njia hizi na utapoteza kila ambacho umekazana kupata.

Kama unataka kujenga uhuru wa kweli kwenye maisha yako, anza na uhuru, chagua kufanya kile tu ambacho ni sahihi, kataa kupokea upendeleo wowote ambao baadaye utatumika kukulazimisha ufanye usiyotaka kufanya.

Hata kama unaanzia chini kabisa na huna kitu, usitumie uhitaji wako kujiingiza kwenye mtego wa utumwa. Kuwa huru na simamia uhuru wako hata kama utakunyima baadhi ya vitu vizuri.

Kumbuka hakuna kitu cha bure, kuna namna utalipa kwa chochote unachopata, hivyo anzia kwenye uhuru kwa kusimama na kilicho sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha