Chochote unachotaka kwenye safari yako ya mafanikio, tayari kipo ndani yako.
Kama unataka mtu wa kukusifu na kukupa moyo wa kuendelea na safari hiyo, hivyo vitu vipo ndani yako. Ni wewe kuangalia ulikotoka na ulipo sasa na kutambua hatua ulizopiga kisha kujisifu na kujipa moyo wa kuendelea kujituma zaidi ili kufanya makubwa zaidi.
Kama unataka mtu wa kumlaumu kwa wewe kushindwa kufanya kile ulichopanga kufanya au kufika ulikotaka kufika, basi mtu huyo yupo ndani yako. Jilaumu wewe mwenyewe, angalia ni maandalizi gani hukuwa nayo au hatua zipi hukuchukua na hilo likapelekea wewe kushindwa. Kwa kufanya hivi utaacha kurudia makosa yako mwenyewe na hivyo kuacha kujizuia kufanikiwa.
Kila kitu kinaanza na wewe mwenyewe na unapoanzia ndani yako unapata nguvu kubwa ya kuendelea na pia unakuwa huru.
Vitu hivi pia unaweza kuvipata kwa wengine, lakini unapovipata kwa wengine, unakuwa tegemezi kwao, unaacha kufanya yale muhimu kwako na hapo unaondoka kwenye njia yako ya mafanikio.
Unapotaka wengine wakusifu na kukupa moyo, unalazimika kufanya vitu vitakavyowafurahisha wao, hata kama havikufikishi wewe kwenye mafanikio. Unaweza ukazipata sifa, lakini hazitakuwa na mchango wowote kwako. Lakini inapoanzia ndani yako, unakuwa huru kufanya yale muhimu kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha kwa hili kila ninachokitafuta kwenye mafanikio ya maisha yangu viko ndani yangu
LikeLike